WATANZANIA WAHAMASISHWA KUTEMBELEA VIVUTIO KUPITIA KAMPENI YA ‘TWENZETU KILELENI’ YA ZARA


DAR ES SALAAM

Watanzania wamehamasishwa kutumia fursa ya utalii wa ndani kwa kutembelea vivutio mbalimbali nchini, huku kampeni ya ‘Twenzetu Kileleni’ ikiingia msimu wake wa tano kwa kulenga kuwapeleka mamia ya wananchi kileleni mwa Mlima Kilimanjaro.

Kampeni hiyo iliyoanzishwa na Zara Tanzania Adventures imezinduliwa Septemba 10, 2026, katika Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam, ikiwa sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 65 ya Uhuru wa Tanganyika yenye kaulimbiu inayosisitiza umoja wa Taifa na kilele cha Afrika.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Zainab Ansell, amesema zaidi ya washiriki 200 wanatarajiwa kupanda Kilimanjaro kupitia njia ya Marangu, huku vijana watakaoungana na kampeni hiyo wakitarajiwa kuongeza idadi ya washiriki hadi zaidi ya 400.

Amesema safari hiyo haitalenga kupanda mlima pekee, bali pia itaunganisha utalii na uhifadhi wa mazingira, ambapo washiriki watashiriki shughuli za upandaji miti kabla ya kuanza safari. Kwa wasioweza kupanda Kilimanjaro, amesema watapata nafasi ya kutembelea Serengeti, Ziwa Manyara na Ngorongoro kwa gharama nafuu.

Ansell amesema Watanzania wanapaswa kutumia kipindi cha Desemba kutembelea vivutio hivyo, akibainisha kuwa wageni kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakifika nchini kwa ajili ya kupanda Kilimanjaro, hivyo wananchi wa ndani wanapaswa pia kujionea utajiri wa rasilimali walizonazo.
Kwa upande wake, Faustin John kutoka Zara Tanzania Adventures amesema maandalizi yamekamilika kwa ajili ya kuhakikisha washiriki wanapata huduma zinazohitajika, zikiwemo malazi, chakula, mavazi, waongoza watalii na elimu ya mazingira. Amesema njia ya Marangu imepewa kipaumbele kutokana na uwepo wa huduma za malazi na mazingira yake kuwa rafiki kwa msimu wa mvua, huku safari ya kufika kileleni ikitarajiwa kuchukua siku sita.

Ofisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Albert Mboto, amesema kampeni hiyo inaunga mkono jitihada za kukuza utalii wa ndani, huku Mary Maduhu kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii akisema wanafunzi na watumishi wa chuo hicho watanufaika kwa kupata uzoefu wa vitendo katika utalii wa milimani, uhifadhi na usimamizi wa urithi wa taifa.

Naye mwakilishi wa TTCL, Peter Mwambuga, amesema kampuni hiyo imeboresha huduma za mawasiliano kuanzia eneo la geti la Marangu hadi kileleni mwa Kilimanjaro, huku John akitoa wito kwa viongozi wa Serikali, wabunge, mawaziri, taasisi binafsi, viongozi wa dini, mabalozi na wananchi kushiriki kampeni hiyo ili kuongeza hamasa ya utalii wa ndani.













Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.