BIDHAA ZA MIGODINI ZAANZA KUZALISHWA NCHINI TANZANIA

📍 Kerege, 

Bagamoyo - Pwani.

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema uzalishaji wa bidhaa zinazotumika katika shughuli za uchimbaji madini nchini ni hatua muhimu katika kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini na kueleza lengo kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa na utengenezaji wa vifaa vya migodini barani Afrika.

Waziri Mavunde ameyasema hayo Oktoba 17, 2026, wakati akizindua rasmi Kiwanda cha kutengeneza Wire Mesh cha Kampuni ya Geofields Tanzania Limited, kupitia Geofields Underground Support (GUS), kilichopo Kerege, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani ili kuongeza uwezo wa Kampuni za Kitanzania kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya migodi nchini na katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo na maono yaliyochangia juhudi za kuimarisha sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa, ikiwemo maelekezo ya kutenga asilimia 10 ya mapato yatokanayo na sekta ya madini kwa ajili ya utafiti wa kina wa madini kwa kutumia fedha za ndani.

Akizungumzia ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta hiyo, Waziri Mavunde amesema Sheria ya Madini inaweka masharti kuhusu ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni za Kitanzania, pamoja na ushirikiano kati ya kampuni za ndani na za kigeni pale ambapo uwezo wa kutoa huduma husika haujajengeka nchini.

Kutokana na hilo, ameiagiza Tume ya Madini kushirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukagua kampuni zilizoingia ubia ili kuthibitisha kuwa zinafanya shughuli zilizosajiliwa na kutimiza masharti yanayotakiwa.

Waziri Mavunde amebainisha kuwa takribani shilingi trilioni 5.1 zilizopo katika mnyororo wa manunuzi wa Sekta ya Madini zinahusishwa na kampuni zisizozidi sita na hivyo kuwahimiza Watanzania kujiandaa kutumia fursa zilizopo kwa kuongeza mitaji, kuunganisha nguvu na kupunguza mgawanyiko wa kibiashara.

Ameiagiza Tume ya Madini kuchunguza namna bora ya kuunganisha Kampuni za Kitanzania ili kuongeza uwezo wao wa kifedha na kiushindani, huku akieleza kuwa Shirika la Mfuko wa Dhamana (Credit Guarantee Scheme Corporation), lililoanzishwa na Benki Kuu ya Tanzania, ni miongoni mwa mifumo inayoweza kusaidia Watanzania kupata fursa zaidi za kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Geofields Tanzania Limited, Denis Dillip, amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha vipande 100,000 vya Wire Mesh kwa mwaka, kiasi ambacho kwa kinauwezo wa kukidhi mahitaji ya migodi nchini.

Dillip ameongeza kuwa Kampuni hiyo inalenga kupanua ushindani wake katika soko la Afrika Mashariki na tayari imefungua tawi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kwamba kiwanda hicho kinazalisha bidhaa zinazolenga kukidhi viwango vya kimataifa na kimeajiri wataalamu waliopata mafunzo ya kitaalamu nchini China na Australia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanislaus Nyongo, amesema mkoa huo una jumla ya viwanda vikubwa na vidogo 1,768, kikiwemo kiwanda cha Geofields, akieleza kuwa uwekezaji huo unaimarisha nafasi ya Pwani kama eneo muhimu la shughuli za viwanda nchini.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amesema Bunge linaendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini na kuitaka kampuni hiyo kutoa kipaumbele kwa wakazi wa Kerege katika fursa za ajira zitakazotokana na uwekezaji huo.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janeth Reuben Lekashingo, amesema mafanikio ya sekta ya madini hayapaswi kupimwa kwa kiasi cha madini kinachochimbwa pekee, bali pia kwa ukuaji wa kampuni za Kitanzania, ajira zinazozalishwa na viwanda vinavyoanzishwa. Amesisitiza kuwa ushirikishwaji wa Watanzania unapaswa kulenga kujenga uwezo wa kampuni za ndani, kuhamisha teknolojia na utaalamu, pamoja na kukuza uzalishaji wa viwandani ili kuongeza manufaa ya sekta ya madini kwa uchumi wa taifa.

Uzinduzi wa kiwanda cha Geofields Tanzania Limited ni sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazotumika migodini ndani ya nchi, kupanua fursa za ajira na kuimarisha uwezo wa Kampuni za Kitanzania kushiriki katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini, huku ukifungua nafasi ya bidhaa zinazozalishwa nchini kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.