Dar es salaam.
Shirika Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake ya ndani kutoka Sh bilioni 1.3 hadi Sh bilioni 147.8 katika mwaka wa fedha 2025/2026, huku likifanikiwa kutoa gawio la Sh bilioni 11 kwa Serikali, ikiwa ni hatua inayotajwa kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1972.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. CPA Venance Mwasse, ameyasema hayo wakati wa kikao kazi kati ya shirika hilo na wahariri wa vyombo vya habari, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na mabadiliko ya kiutendaji, uwekezaji katika miradi ya madini na kuimarisha uwajibikaji ndani ya shirika.
Amesema STAMICO imefanyiwa mageuzi ya kiutendaji na kibiashara ili kuwa shirika lenye uwezo wa kuwekeza, kuzalisha mapato na kushindana katika sekta ya madini, baada ya kupitia changamoto zilizotokana na mabadiliko ya sera za ubinafsishaji kuanzia mwaka 1997.
Amesema shirika hilo lililofufuliwa mwaka 2010 lilikabiliwa tena na changamoto zilizohatarisha uendelevu wake, hali iliyosababisha kuanzishwa kwa mabadiliko ya kuimarisha miradi, kuongeza uwajibikaji na kuweka mifumo ya kupima utendaji wa viongozi na watumishi.
Dkt. Mwasse amesema katika mageuzi hayo, STAMICO imeweka kipaumbele katika kuwajengea uwezo watumishi, kuboresha ushirikiano na Wizara ya Madini, Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na wadau wengine, akisisitiza kuwa rasilimali watu ni msingi wa mafanikio ya shirika.
Ameeleza kuwa STAMICO inaendelea kutekeleza miradi inayohitaji mtaji na teknolojia kubwa, ikiwemo uchimbaji wa makaa ya mawe, uchorongaji wa miamba, uzalishaji wa nishati safi ya kupikia kupitia bidhaa za Rafiki Briquette pamoja na uwekezaji katika dhahabu na madini mkakati kama grafiti na nikeli.
Kuhusu uchorongaji, amesema shirika lina mitambo 18 inayotumika kutoa huduma kwa wateja mbalimbali, wakiwemo kampuni za Geita, Shanta katika maeneo ya Singida na Chunya, GFX na Nyanza, hatua inayolenga kuongeza mapato na kupanua huduma katika sekta ya madini.
Katika eneo la nishati safi ya kupikia, amesema STAMICO imeanzisha viwanda vitano vya Rafiki Briquette katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Kisarawi, Kiwira, Dar es Salaam na Tabora, huku ikiendelea na maandalizi ya uzinduzi wa kiwanda kingine kikubwa kinachotajwa kuwa miongoni mwa vikubwa Afrika Mashariki.
Aidha, amesema shirika limeelekeza nguvu katika kuendeleza miradi ya dhahabu na madini mkakati pamoja na kushiriki katika ubia na kampuni mbalimbali ili kuongeza thamani ya rasilimali za madini na kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na sekta hiyo.
Dkt. Mwasse amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa kubadili mtazamo wa uendeshaji wa mashirika ya umma kutoka kutegemea zaidi msaada kwenda katika uwekezaji unaozalisha mapato, ajira na faida kwa taifa.
Amesema STAMICO itaendelea kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria, ikiwemo kuwalea, kuwaendeleza, kuwasaidia na kuwarasimisha wachimbaji wadogo wa madini wenye leseni za uchimbaji mdogo, ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya uchumi.
Ameeleza kuwa maono ya shirika hilo ni kuhakikisha linakuwa taasisi yenye ushindani na inayoweza kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa madini, akitaja kauli mbiu ya mageuzi hayo kuwa “Make STAMICO Shine Again”, ikiwa na lengo la kulifanya shirika liwe imara, lenye tija na lenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania.






Hakuna maoni: