Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM.
Rais wa Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ), Omar Faruk Osman, ameitaka Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kuongeza kasi ya kusajili wanachama ili kujenga nguvu na ushawishi wa chama hicho ndani na nje ya Tanzania.
Omar ametoa kauli hiyo Oktoba 6, 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya, pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Said Mmanga.
Amesema JOWUTA ni miongoni mwa vyama vya wafanyakazi wa vyombo vya habari vinavyokua kwa kasi, hivyo kinapaswa kuongeza juhudi katika usajili wa wanachama kwa kuwa idadi kubwa ya wanachama ni msingi wa nguvu ya chama cha wafanyakazi.
Amesema FAJ inaitazama Tanzania kama nchi ya kimkakati kutokana na ushawishi wake katika masuala mbalimbali barani Afrika, hivyo JOWUTA inapaswa kuwa na nguvu inayotokana na idadi ya wanachama wake.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa JOWUTA kulipa ada na michango yake katika Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ) kwa wakati ili kuendelea kunufaika na fursa mbalimbali, ikiwamo kushiriki mikutano, mafunzo na miradi ya maendeleo.
“Nashukuru sana kwa kuonana na nanyi hapa. Mwenyekiti ameniambia yupo Nairobi kikazi. Endeleeni kusajili wanachama wapya na kulipa ada kwa wakati ili muwe hai ndani ya IFJ na kupata nafasi ya kushiriki mikutano, mafunzo na miradi ya maendeleo inayoendeshwa na FAJ,” amesema.
Omar ameipongeza JOWUTA kwa kuanzisha programu ya kuhamasisha waandishi wa habari walio katika mfumo rasmi na wale walio nje ya mfumo huo kujiunga na utaratibu wa Hifadhi ya Jamii kwa Hiari unaotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Pia amekitaka chama hicho kuendelea kutoa mafunzo kwa wanachama wake kila kinapopata fedha, akisema hatua hiyo itasaidia kuvutia waandishi wengi zaidi kujiunga na JOWUTA.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya, amemshukuru Omar kwa kutenga muda wa kukutana nao na kusisitiza kuwa chama kitaendelea na usajili wa wanachama katika NSSF na mifuko mingine ya hifadhi ya jamii ili kuimarisha usalama wa maisha ya waandishi wa habari baada ya ajira.
Msuya ameahidi kushirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha wanaongeza idadi ya wanachama na kulipa ada kwa wakati, kama taratibu zinavyoelekeza.
Aidha, ameiomba FAJ kutenga bajeti kwa ajili ya kuendesha mafunzo kwa waandishi wa habari nchini Tanzania.

Hakuna maoni: