KITUO CHA TAARIFA CHA NANDETE KUPATA MSUKUMO MPYA, JIWE LA MSINGI LAWEKWA KATIKA KILELE CHA KUMBUKIZI YA MIAKA 121 YA VITA VYA MAJI MAJI

KILWA, Lindi, Oktoba 4, 2026

SERIKALI imeendelea kuweka msukumo katika kuhifadhi na kuendeleza historia ya Vita vya Maji Maji, baada ya kuweka jiwe la msingi la Kituo cha Taarifa cha Nandete, Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi.

Kituo hicho kinatarajiwa kukamilika mwaka 2027 na kuwa sehemu muhimu ya kutoa taarifa kuhusu historia, utamaduni na urithi wa eneo hilo, pamoja na kuchochea utalii wa urithi.

Jiwe la msingi liliwekwa jana katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 121 ya Kumbukizi ya Vita vya Maji Maji, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla iliyowakutanisha viongozi, wananchi, wazee wa mila na wadau mbalimbali wa uhifadhi wa historia na urithi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Nyundo amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha historia na urithi wa mashujaa wa Vita vya Maji Maji unatunzwa, kuhifadhiwa na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema kituo hicho kitakuwa na umuhimu katika kutoa taarifa na kuibua historia ya Vita vya Maji Maji, hususan matukio yaliyohusisha eneo la Nandete, huku kikitarajiwa pia kuchochea shughuli za utalii na kukuza uchumi wa wananchi.

Mhe. Nyundo amewataka wananchi kutumia fursa zitakazotokana na uwekezaji huo, ikiwemo kuendelea kujenga nyumba za kulaza wageni na kuboresha huduma mbalimbali ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea Nandete na kunufaisha jamii kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, amewashukuru wananchi wa Nandete na Kilwa kwa kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo na kushiriki katika juhudi za kuhifadhi historia ya Vita vya Maji Maji.

Dkt. Lwoga amesema mwitikio wa wananchi unaonesha umuhimu wa historia ya Vita vya Maji Maji katika jamii, akisisitiza kuwa ushirikiano wao ni msingi wa kuhakikisha urithi huo unahifadhiwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.

Amesema Kituo cha Taarifa cha Nandete kitakapokamilika kitakuwa nyenzo muhimu ya kutoa elimu kwa wananchi, wanafunzi, watafiti na wageni kuhusu historia ya Vita vya Maji Maji, pamoja na kuimarisha utalii wa urithi katika eneo la Kilwa.

“Tunawashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kulipokea suala hili. Ushiriki wenu unaonesha wazi kwamba historia hii ni ya wananchi na inapaswa kuhifadhiwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo,” amesema Dkt. Lwoga.

Maadhimisho hayo ya miaka 121 yamefanyika chini ya kaulimbiu ‘Maji Maji na Urithi wa Kilwa’, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuenzi mashujaa wa Vita vya Maji Maji, kuimarisha uhifadhi wa maeneo ya kihistoria na kutumia urithi wa Kilwa kama fursa ya kukuza utalii, elimu na uchumi wa jamii.

Kuwekwa kwa jiwe la msingi la Kituo cha Taarifa cha Nandete kunatarajiwa kuongeza msukumo katika uhifadhi wa historia na urithi wa eneo hilo, huku kituo hicho kikitarajiwa kukamilika mwaka 2027.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.