DAR ES SALAAM.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema hali ya usalama jijini humo ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku bila bughudha.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kaimu Kamanda Faustine Mafwele amesema Jeshi hilo limejiandaa kikamilifu kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga utakaochezwa Jumamosi, Oktoba 10, 2026, katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Amesema ulinzi na usalama umeimarishwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, huku akiwataka mashabiki wa timu hizo kuzingatia sheria, kanuni za soka na taratibu za mikusanyiko ili kuhakikisha mchezo huo unafanyika kwa amani na utulivu.
Katika hatua nyingine, Jeshi hilo limethibitisha kupatikana kwa Angel Abayo, mwenye umri wa miaka 19, aliyekuwa akifanya kazi za ndani na ambaye alidaiwa kutoweka akiwa na mtoto mdogo kutoka eneo la Kigamboni Kibada.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, Angel aliondoka na mtoto huyo kwenda Kibaha kumtembelea dada yake aliyepata ajali, baada ya mwajiri wake kumkatalia ruhusa ya kwenda kumwona ndugu yake huyo. Polisi wamewashukuru wananchi na wadau wa upelelezi kwa ushirikiano wao uliowezesha kupatikana kwa mtoto huyo.
Aidha, Mafwele amewakaribisha wananchi na waandishi wa habari kushiriki katika kampeni ya “Ongea na Kamanda”, inayolenga kuwakutanisha viongozi wa Polisi na wananchi katika maeneo yao kwa ajili ya kusikiliza changamoto za kiusalama, kupokea maoni na kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa kero zinazowakabili.
Amesema ushiriki wa waandishi wa habari katika mikutano hiyo ni muhimu katika kuibua na kufikisha changamoto za wananchi kwa mamlaka husika.

Hakuna maoni: