MHE. MMUYA ATOA KONGOLE KWA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI MSUMBIJI KWA KUENDELEA KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI
Na, Mwandishi wetu
Maputo, Msumbiji
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya ameupongeza Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji kwa namna unavyoendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kutangaza fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Msumbiji.
Mhe. Mmuya ametoa pongezi hizo alipotembelea ofisi hizo pamoja na ujumbe alioongozana nao kwa lengo la kushiriki Kongamano la Usimamizi wa Maafa kuhusu Kupunguza Hatari za Maafa na Kuimarisha Ustahimilivu wa Bara la Afrika dhidi ya majanga kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.Kongamano hilo linalofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 13 hadi 15 Oktoba, 2026 Jijini Maputo Nchini Msumbiji
Amesema kuwa, Ubalozi huo, chini ya uongozi wa Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo unazidi kufungua milango ya ushirikiano wa kimkakati katika sekta za kipaumbele ikiwemo Biashara na Uwekezaji kwa kushirikisha kampuni za Kitanzania katika sekta mbalimbali kama vile sekta ya mafuta, gesi, na nishati na kuhamasisha ushiriki wao katika soko la Msumbiji.
“Mmeendelea kufanya kazi nzuri yenye tija kwa Taifa letu kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia maeneo ya usafirishaji wa baharini na maendeleo ya bandari ili kurahisisha mzunguko wa mizigo, hii inaimarisha diplomasia yetu na nchi ya Msumbiji,” alisema Mhe. Mmuya
Akitoa taarifa kuhusu Ofisi za Ubalozi huo, Mheshimiwa CP. Balozi Hamad amesema wameendelea kuhakikisha wanaimarisha diplomasia kwa kuzitangaza fursa zilizopo na kuendelea kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili.
Aidha Balozi Hamad amemshukuru Naibu Waziri Mmuya kwa kutenga muda na kutembelea ofisi hizo na kusema kuwa, wataendelea kuiwakilisha vyema Nchi ya Tanzania na kuitangaza ili kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji waje nchini kuwekeza.
AWALI
Kongamano la Usimamizi wa Maafa kuhusu Kupunguza Hatari za Maafa na Kuimarisha Ustahimilivu wa Bara la Afrika dhidi ya majanga hilo limeandaliwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Msumbiji pamoja na Sekretarieti ya SADC. Kaulimbiu ya Kongamano hilo ni “Kuimarisha Utawala katika Usimamizi wa Maafa na Uwekezaji wa Kimkakati ili kupunguza hatari za Maafa na kujenga Afrika imara inayostahimili majanga"



Hakuna maoni: