Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema hakuna mfanyabiashara atakayezuiwa kufanya biashara, lakini amesisitiza kuwa barabara haziruhusiwi kutumika kama maeneo ya biashara. Amesema wafanyabiashara wanapaswa kuondoa meza na bidhaa barabarani, kwa kuwa barabara zinahitajika kwa matumizi ya wananchi, magari ya dharura kama zimamoto, ambulance n.k., na pia kulinda usalama wa maeneo husika.
Akizungumzia hali ya biashara jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema Kariakoo ni eneo la kimkakati kikodi, hivyo linapaswa kusimamiwa kwa sheria na utaratibu. Amesema hadi tarehe 24 Oktoba 2026, barabara za Kariakoo zinapaswa kuwa zimefunguliwa na kutotumika kwa shughuli za biashara, akisisitiza: “Ondoa meza, fungua barabara.”
Ameeleza kuwa kuziba barabara kuna madhara kadhaa, ikiwemo kushusha thamani ya majengo yaliyowekezwa, kuchochea ukwepaji wa kodi na hivyo kupunguza mapato ya Serikali. Aidha, endapo litatokea janga la moto, kuzibwa kwa barabara kunaweza kuchelewesha magari ya zimamoto kufika kwenye jengo husika. Amesema hali hiyo pia huharibu mwonekano wa soko na kulifanya lionekane chafu na lisilo na mpangilio. Kwa msingi huo, Chalamila amesisitiza kuwa Dar es Salaam lazima isimamiwe kwa sheria katika biashara ndogondogo na kubwa.

Hakuna maoni: