SERIKALI KUKAGUA UMILIKI WA KAMPUNI ZA HUDUMA MIGODINI


GEITA

Serikali kupitia Tume ya Madini inatarajia kuanza kuhakiki umiliki halali wa kampuni zinazotoa huduma kwenye migodi ya madini nchini, ili kuhakikisha fursa za ajira, huduma na biashara zinawanufaisha Watanzania wenye sifa na uwezo unaohitajika.

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti utaratibu unaodaiwa kuwepo wa kampuni za kigeni kuingia ubia na Watanzania wasio na sifa stahiki kwa ajili ya kutimiza matakwa ya ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini.

Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo mapema leo Oktoba 2, 2026, wakati akifungua Siku ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya Kitaifa ya Tisa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bomba Mbili, Geita.

Amesema katika utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, imebainika kuwepo kwa kampuni za kigeni zinazoingia ubia na Watanzania kwa lengo la kutimiza matakwa ya umiliki wa hisa, wakati kiuhalisia kampuni hizo zinamilikiwa na wageni.


“Nimebaini kumekuwepo na kampuni za kigeni ambazo zimekuwa zikiingia ubia na Watanzania ambao wanatakiwa kuwa na asilimia 20 ya hisa kimaandishi, lakini ukija kiuhalisia unabaini kampuni inamilikiwa na wageni pekee,” amesema.

Amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali ikiwemo BRELA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), itahakiki umiliki wa kampuni hizo pamoja na miamala inayofanyika ili kubaini umiliki halali wa kampuni husika.

Waziri Mavunde pia amewataka Watanzania kujiandaa kuchangamkia fursa za kutoa huduma na bidhaa kwenye migodi, akisema kampuni 14 zinatarajiwa kuanza shughuli za uchimbaji wa madini, huku leseni nyingine 28 zikiwa katika hatua za kutolewa.

Amesema ongezeko hilo linatarajiwa kuongeza mahitaji ya huduma na bidhaa mbalimbali migodini, hivyo kuwataka watoa huduma wa ndani kujiandaa na, pale inapowezekana, kuungana ili kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji makubwa ya kampuni za uchimbaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesema Serikali imeanza kutekeleza mkakati wa kutumia asilimia 10 ya makusanyo ya maduhuli yatokanayo na Sekta ya Madini kwa ajili ya shughuli za utafiti wa madini.

Amesema katika kipindi cha miezi mitatu ya mwaka wa fedha 2026/2027, kuanzia Julai hadi Septemba, Wizara kupitia Tume ya Madini ilikusanya shilingi bilioni 411, sawa na asilimia 117 ya lengo la shilingi bilioni 351.

“Katika makusanyo hayo, kiasi cha shilingi bilioni 40, sawa na asilimia 10, kitaanza kutumika katika shughuli za utafiti wa madini,” amesema.

 


Ameongeza kuwa Serikali pia imetenga eneo lililokuwa likitumika na Mgodi wa Buzwagi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vitakavyozalisha bidhaa zinazohitajika katika shughuli za migodini, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini.


Aidha, amesema Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 90 ya manunuzi ya kampuni za madini, yenye thamani ya takribani shilingi trilioni 5.1 kwa mwaka, yanafanywa na Watanzania ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika kukuza uchumi wa nchi.


Waziri Mavunde pia amewapongeza wachimbaji wadogo kwa mchango wao unaofikia asilimia 40 katika Sekta ya Madini, akisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali ilikusanya shilingi trilioni 1.393 kutokana na shughuli za sekta hiyo.

Amesema utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini umeendelea kuleta matokeo, ikiwemo kuongezeka kwa ajira rasmi 19,000, huku raia wa kigeni wakichangia asilimia nne ya ajira katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amewataka Watanzania kuacha kulalamika kuhusu fursa zilizopo na badala yake kuwa wabunifu na kuzichangamkia ili kuongeza ushiriki wao katika Sekta ya Madini.

Mbunge wa Geita, Chacha Wambura, ameiomba Wizara ya Madini kuendelea kusimamia kwa nguvu utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, huku ikiendelea kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo nchini.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo, pamoja na kufanya maboresho ya Sheria na Kanuni za Madini.

Awali, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, amesema mkutano huo uliowakutanisha wamiliki wa leseni za madini na watoa huduma kwenye migodi unalenga kubadilishana uzoefu, kutoa elimu, kuweka mikakati ya ushirikiano na kubuni njia bora za kutatua changamoto zinazowakabili wadau wa Sekta ya Madini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.