SERIKALI YAWEKEZA MABILIONI KUBORESHA HUDUMA ZA TBS

DAR ES SALAAM

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa viwango 3,901 vya bidhaa na kutoa vyeti na leseni za ubora 3,940 kwa wazalishaji, wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,683, katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, ameeleza hayo Oktoba 27, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao kazi cha Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichowakutanisha waandishi wa habari na wahariri. Amesema hatua hizo zinalenga kuboresha ubora na usalama wa bidhaa za ndani na kuwawezesha wazalishaji kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Katunzi amesema shirika hilo limeendelea kuimarisha ukaguzi na usajili wa bidhaa, maeneo ya biashara na kutoa elimu kwa wazalishaji kuhusu viwango na ubora kwa kuzingatia Sheria ya Viwango, Sura ya 130. Ameongeza kuwa Serikali imewekeza katika miundombinu ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Amesema ujenzi wa ofisi na maabara za TBS katika eneo la Njedengwa, Dodoma, kupitia mradi wa Viwango House–Dodoma wenye thamani ya shilingi bilioni 24.7, umefikia hatua za mwisho za ukamilishaji na makabidhiano. Vilevile, ujenzi wa kituo cha Viwango House–Mwanza katika eneo la Kiseke, Wilaya ya Ilemela, unaendelea kwa gharama inayokadiriwa kuwa shilingi bilioni 12.1, huku maandalizi ya ujenzi wa kituo kingine Arusha yakiwa katika hatua za awali.

Amesema maabara za Dodoma zinatarajiwa kuhudumia mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora, wakati kituo cha Mwanza kitahudumia mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu. Uwekezaji huo unalenga kupunguza gharama za upimaji na kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa majibu ya sampuli.

Aidha, Serikali kupitia TBS imetumia zaidi ya shilingi bilioni 9.8 kuboresha ofisi tisa za kanda pamoja na ofisi zilizopo mipakani, bandarini na viwanja vya ndege. Uboreshaji huo umehusisha kuongeza ofisi, watumishi na vifaa vya kazi ili kuimarisha ukaguzi wa bidhaa na kudhibiti bidhaa zisizokidhi viwango, kwa lengo la kulinda afya na usalama wa walaji.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.