
Na mwandishi wetu,
Dar es Salaam.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linatarajia kufunga Mashine Umba (Transfoma) jipya yenye uwezo wa MVA 120, itakayoongeza uwezo wa kituo cha kupokea na kupoza Umeme cha Dege na kusaidia kukidhi mahitaji na kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme kwa Wananchi katika Mkoa wa Ki - TANESCO, Kigamboni.
Mashine Umba (Transfoma) hiyo imewasili katika eneo la ujenzi wa kituo cha Dege, ikiwa ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mradi wa upanuzi wa Kituo hicho wenye thamani ya takribani Sh. Bilioni 17 unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania, kupitia TANESCO.
Akielezea umuhimu wa utekelezaji wa Mradi huo kwa niaba ya Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kimbiji Mhandisi Lukaluka Kapinga amesema kituo hicho kilikuwa kikitegemea Transfoma yenye uwezo wa MVA 60, ambayo ilikuwa ilikabiliwa na ongezeko la mahitaji ya umeme, hali iliyochangia changamoto ya huduma kwa baadhi ya wateja.
“Kuongezeka kwa uwezo wa Transfoma kutoka MVA 60 hadi MVA 120 kutaimarisha uwezo wa kituo chetu na kukidhi mahitaji ya umeme kwa Wananchi wetu wa Kigamboni, ambapo maboresho haya yanatarajiwa kuongeza uwezo wa kituo kwa kiwango kikubwa na kusaidia kupunguza changamoto zinazotokana na ongezeko la matumizi ya umeme,” amesema Mha. Kapinga.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa ufungaji na majaribio ya kiufundi, Transfoma hiyo itakuwa tayari kuanza kazi, hatua itakayosaidia kuboresha huduma ya umeme kwa wananchi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali zinazotegemea nishati hiyo katika shughuli zao za kila siku.
Aidha Mhandisi Lukaluka amewaomba wananchi wa Kigamboni kuendelea kuwa wavumilivu wakati kazi ya utekelezaji wa Mradi huo ukiendelea kwa kasi kubwa ili kuimarisha miundombinu ya umeme na kuongeza uwezo wa kukidhi mahitaji yanayoendelea kukua kutokana na maendeleo ya makazi na shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Kigamboni
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa upanuzi wa Kituo cha kupokea na kupoza Umeme cha Dege Mhandisi Edward Ngalamika amesema hadi sasa, Mradi huo umefikia asilimia 79.3 ya utekelezaji wake, ambapo ufungaji na majaribio ya Mashine Umba hiyo (Transfoma) hiyo ukitarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 22, 2026.
Amesema kukamilika kwa ufungaji wa Transfoma hiyo kunatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wakazi na wafanyabiashara wa Kigamboni, hasa ambao shughuli zao zinategemea huduma ya umeme.
“Tunatarajia ufungaji na majaribio ya transfoma hii kukamilika ifikapo Desemba 22, 2026, ambapo maboresho haya yatasaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme na kurahisisha shughuli za kila siku kwa wakazi wa Kigamboni,” amesema Mha. Ngalamika
Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali na TANESCO za kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme kwa Watanzania katika Maeneo mbalimbali nchini.



Hakuna maoni: