Na Beatus Maganja, Zanzibar
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inaangalia uwezekano wa kuanzisha utalii wa mchezo wa gofu katika eneo linalopendekezwa kuanzishwa Zanzibar Wildlife Park ndani ya Msitu wa Hifadhi ya Jambiani Muyuni, Zanzibar ili kuongeza zao jipya la utalii na kuvutia wageni kutoka masoko mapya.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis R. Semfuko, ameeleza hayo Oktoba 21, 2026, wakati wa ziara ya wataalamu wa Troon International, kampuni yenye.makao makuu nchini Marekani inayosimamia viwanja vya gofu na klabu katika mataifa mbalimbali. Ujumbe huo umetembelea eneo hilo kutathmini uwezekano wa kuanzisha uwanja wa gofu, fursa za uwekezaji na namna ya kushirikiana katika uendeshaji wake.
“Gofu ni mchezo ambao unaleta watalii wengi,” amesema Meja Jenerali Semfuko, akieleza kuwa wataalamu hao wamefika kwa mara ya kwanza kujionea eneo hilo na kupata taarifa zitakazowawezesha kutoa ushauri kuhusu uwezekano wa kuendeleza uwanja wenye viwango vya kimataifa.
Amesema dhamira ya TAWA ni kuunganisha utalii wa gofu na utalii wa picha ili kupanua shughuli za kitalii katika eneo hilo. Ameongeza kuwa ushauri wa wataalamu hao utasaidia kubaini namna ya kuendeleza gofu kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na mahitaji ya soko la utalii.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mtendaji wa Troon International David Jonathan amesema uwepo wa uwanja wa gofu katika eneo lenye wanyamapori unaweza kuiongezea Zanzibar kivutio cha kipekee kwa wachezaji wanaopenda kuchanganya mchezo huo na kutembelea vivutio vya utalii.
Jonathan amesema utalii wa gofu unaweza kuongeza muda wa watalii kukaa nchini na huku wakifurahia fukwe, wanyamapori, utamaduni na vyakula vya Zanzibar. Aidha, amesema uwanja wenye viwango vya kimataifa unaweza kuvutia mashindano na kusaidia kuitangaza Zanzibar katika masoko ya utalii wa gofu.
Naye Mhandisi Ujenzi kutoka TAWA, Samuel Hagu amesema wazo la kuanzisha uwanja wa gofu wa kiwango cha mashindano, unaojulikana kitaalamu kama championship course, linalenga kuongeza kivutio kingine katika mradi wa Zanzibar Wildlife Park na kuwapa wageni wigo mpana wa shughuli za kitalii.
Hagu amesema mpango unaopendekezwa unahusisha pia uwepo wa wanyamapori mbalimbali na michezo kwa watu wa rika zote, huku msitu ukiendelea kuhifadhiwa. Majadiliano kati ya TAWA na Troon International yanatarajiwa kuendelea ili kubainisha mahitaji ya kitaalamu, uwezekano wa uwekezaji na hatua zitakazofuata katika kuendeleza wazo hilo.







Hakuna maoni: