DAR ES SALAAM.
Kampuni ya Amesco Truck Parts, inayojihusisha na uuzaji na usambazaji wa vipuri vya magari, imeibuka mshindi wa tuzo ya kampuni bora ya mwaka katika biashara ya vipuri vya magari kwenye tuzo za Best Brand Awards 2026.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa kampuni hiyo Novemba 14, 2026, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuenzi chapa zinazofanya vizuri sokoni na kupata uungwaji mkono wa wananchi.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Aristides Mbwasi, katika hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa biashara na sekta ya viwanda.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Amesco Truck Parts, Amiri Mkufya, amewashukuru Watanzania kwa kuendelea kuiamini kampuni hiyo na kuipigia kura, akisema ushindi huo ni matokeo ya imani waliyoijenga kwa wateja wao.
Amesema tuzo hiyo si sababu ya kusherehekea mafanikio pekee, bali ni chachu ya kuendelea kuboresha huduma na kuhakikisha kampuni inatoa bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya wateja.
"Kwetu sisi hii si tuzo ya kusherehekea mafanikio, bali inatupa chachu ya kuongeza ubora wa huduma na bidhaa zetu, huku tukilenga kuwa chapa namba moja barani Afrika. Ubora wa bidhaa zetu utaendelea kuwa sehemu muhimu ya misingi ya kampuni yetu," amesema Mkufya.
Tuzo za Best Brand Awards zinaandaliwa na kampuni ya Best Brand Africa inayoongozwa na Zakayo Shushu, zikilenga kutambua kampuni na chapa zinazofanya vizuri sokoni na kupata umaarufu pamoja na kuaminiwa na watumiaji kupitia mfumo wa People's Choice.


Hakuna maoni: