KAMATI YA KITAIFA YA UFUNGAJI MIGODI YAPITIA MPANGO WA UFUNGAJI MGODI WA DHAHABU WA BUCKREEF

KATORO, GEITA.

Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi imepitia Mpango wa Ufungaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef uliopo mkoani Geita, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha shughuli za ufungaji wa mgodi huo zitakapofika wakati wake zinafanyika kwa kuzingatia sheria, usalama, afya na utunzaji wa mazingira.

Hatua hiyo inalenga kuutathmini mpango huo kitaalamu kabla ya kuidhinishwa na kuweka msingi wa utekelezaji wake kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123, pamoja na Kanuni za Madini (Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira) za mwaka 2010.

Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika Katoro, Geita, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema migodi yote mikubwa na ya kati ina wajibu wa kisheria kuandaa mipango ya ufungaji migodi na kuiwasilisha kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi kwa ajili ya mapitio ya kitaalamu kabla ya kuidhinishwa na kamati hiyo.

Amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 206 ya Kanuni za Madini (Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira) za mwaka 2010, wamiliki wa migodi wanapaswa kuandaa mipango hiyo ili kuhakikisha kuwa shughuli za ufungaji migodi zinapofika wakati wake zinatekelezwa kwa utaratibu unaozingatia matakwa ya kisheria.

Mhandisi Kamando amefafanua kuwa jukumu la kamati hiyo si kuamua kufungwa kwa mgodi kabla ya kumaliza rasilimali zake za madini, bali ni kupitia na kutathmini mipango ya ufungaji mapema ili kuhakikisha kuwa migodi inapofikia mwisho wa shughuli zake, inafungwa kwa kuzingatia usalama wa watu na kurejesha mazingira katika hali salama.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef, Isaac Busanseba, ameihakikishia kamati hiyo kuwa uongozi wa mgodi unaendelea kuzingatia matakwa ya usalama, afya na utunzaji wa mazingira katika shughuli zake.

Amesema mgodi huo utazingatia maelekezo na mapendekezo yote yatakayotolewa na kamati ili kuhakikisha kuwa mpango wa ufungaji mgodi unakidhi matakwa ya kisheria na viwango vinavyotakiwa.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Madini, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Tume ya Madini pamoja na wawakilishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya ya Geita.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.