Mafia - Pwani
Utalii wa samaki aina ya Papa Potwe umeingizia uchumi wa Kisiwa cha Mafia mkoani Pwani Sh bilioni 9.5 mwaka 2025, huku idadi ya samaki hao ikiongezeka kutoka 100 mwaka 2012 hadi kufikia zaidi ya 268 mwaka 2025.
Kiongozi wa Mtandao wa Waongoza Watalii wa Papa Potwe Tanzania (WATON), Baraka Kilopola, amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za uhifadhi, elimu kwa jamii na ushirikiano kati ya taasisi zinazohusika na Serikali pamoja na wavuvi. Amesema mtandao huo unatoa elimu ya mazingira kwa wananchi, wavuvi na wanafunzi ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuwalinda samaki hao.
Amesema WATON imejikita katika uhifadhi wa Papa Potwe kwa sababu za kiuchumi na kisayansi, akieleza kuwa samaki huyo ni mkubwa kuliko wote duniani, lakini hana meno wala haumi binadamu. Hali hiyo huwavutia watalii wanaopata fursa ya kuogelea karibu naye, huku ukubwa wake na madoa yaliyopo mwilini mwake vikiongeza mvuto wa shughuli hiyo.
Kilopola amesema awali wananchi walidhani Mafia kuna Papa Potwe kati ya wanane na 10 pekee, lakini utafiti uliofanywa mwaka 2012 na shirika la Marine Megafauna kwa kushirikiana na WWF na Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ulibaini kuwepo kwa samaki hao 100 na zaidi. Utafiti wa mwaka 2025 umeonyesha idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 268, hali inayohusishwa na mazingira salama, elimu kwa jamii na ushirikiano wa wadau wa uhifadhi.
Ameeleza kuwa kila mtalii anayefika Mafia kwa ajili ya kuwaona Papa Potwe hutumia kati ya Dola za Marekani 1,000 na 1,500. Kutokana na shughuli hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imekusanya zaidi ya Sh milioni 100 kupitia tozo za uhifadhi, huku fedha nyingine zikizunguka katika mnyororo wa thamani unaohusisha hoteli, waongoza watalii, kampuni za ndege na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Amesema uwepo wa samaki hao kwa wingi katika eneo hilo unachangiwa pia na mazingira ya kijiografia ya Mafia, ambacho kiko karibu na Mto Rufiji. Mto huo huleta chakula, ikiwemo uduvi, huku umbo la eneo la Kilindoni linalofanana na herufi V likisaidia chakula hicho kukaa kwa muda mrefu na kuwavutia Papa Potwe.
Kilopola amesema Mafia ni eneo la kipekee Tanzania na Afrika kwa urahisi wa kuwaona Papa Potwe kutokana na utalii endelevu unaozingatia miongozo ya kuogelea na samaki hao. Ameongeza kuwa utafiti wa mwaka 2025 umebaini kuwa samaki hao, ambao husafiri umbali mrefu, sasa wanaweza kuonekana Mafia kuanzia Julai hadi Aprili, tofauti na ilivyokuwa awali walipoonekana zaidi kati ya Oktoba na Februari.
Kwa sasa, zaidi ya watalii 6,000 hutembelea Mafia kila mwaka kwa lengo la kuwaona Papa Potwe, wengi wao wakiwa wageni kutoka nje ya nchi. Kilopola amewahimiza Watanzania na wageni kutoka Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani kutembelea kisiwa hicho, akisema Papa Potwe ni sehemu ya fahari ya Mafia na Tanzania. Ameeleza kuwa samaki hao wanaweza kufikia urefu wa mita 18 duniani, huku wanaoonekana Mafia wakiwa na urefu wa mita tatu hadi nane.



Hakuna maoni: