MIRADI YA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME DAR ES SALAAM YAFIKIA HATUA ZA MWISHO KUKAMILIKA – MD TWANGE
Dar es Salaam.
Wananchi wa Dar es Salaam na mikoa jirani wanatarajiwa kupata huduma ya umeme iliyoimarika kufuatia miradi mikubwa ya usafirishaji na usambazaji umeme inayotekelezwa na Serikali kufikia hatua za mwisho za ukamilishaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema hayo Novemba 20, 2026, wakati akikagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya umeme jijini Dar es Salaam, akibainisha kuwa Serikali imewekeza zaidi ya Sh bilioni 193 katika kuimarisha miundombinu hiyo Dar es Salaam na Pwani.
Amesema miradi hiyo inalenga kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka vituo vya uzalishaji hadi kwa watumiaji, ili kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi, viwanda na uwekezaji.
Twange ametaja miradi inayokaguliwa kuwa ni njia ya kusafirisha umeme ya Kimara–Mabibo–Ilala, njia ya umeme wa chini ya ardhi kutoka Kinyerezi hadi Gongo la Mboto, upanuzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Dege, Kigamboni, pamoja na ujenzi wa kituo cha kisasa cha kupokea na kupoza umeme cha Mabibo.
Amesema kwa sasa Dar es Salaam na Pwani zinatumia takribani megawati 800, huku mahitaji yakitarajiwa kufikia megawati 900 kutokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi na kijamii. Ameongeza kuwa baadhi ya miradi inatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu na mingine mwishoni mwa Januari 2027.
Kwa mujibu wa Twange, upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Dege umefikia asilimia 90.4, ujenzi wa kituo cha Mabibo umefikia asilimia 94, huku njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 132 kutoka Kinyerezi hadi Gongo la Mboto ikiwa imefikia asilimia 86.
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali kuimarisha huduma ya umeme na kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo. Serikali pia inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini kutoka takribani megawati 4,600 hadi 4,700 zilizopo sasa na kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.




Hakuna maoni: