DAR ES SALAAM.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wananchi kutokuwa na hofu wanapoyaona magari ya vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali ya jiji, akieleza kuwa uwepo wake ni sehemu ya hatua za kuendelea kulinda amani, usalama na utulivu wa mkoa huo.
Chalamila amesema Dar es Salaam ni miongoni mwa maeneo yenye mwingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli za kiuchumi, kijamii na kibiashara, huku kila siku watu wapya wakiingia kutoka mikoa mingine nchini na nje ya Tanzania, hali inayohitaji kuimarishwa kwa ulinzi na usalama ili kuhakikisha shughuli za wananchi zinaendelea bila kuvurugika.
Amesema uwepo wa vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali ya jiji usitafsiriwe kama sababu ya wananchi kuwa na wasiwasi, bali ni sehemu ya utaratibu wa kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa salama kwa wakazi, wafanyabiashara na wageni wanaofika jijini humo.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa amewashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa kuendelea kuthamini amani na utulivu, akiwataka kudumisha mshikamano na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda mazingira ya amani.
Katika hatua nyingine, Chalamila ameonya kuwa vitendo vya vurugu vinaweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Dar es Salaam, hususan katika upatikanaji na usambazaji wa chakula pamoja na shughuli za biashara.
Amesema kwa kuwa Dar es Salaam haitegemei uzalishaji wa kilimo kwa kiwango kikubwa, mkoa huo hutegemea chakula kinacholetwa kutoka mikoa mingine, hivyo kuvurugika kwa usafirishaji na biashara kunaweza kuathiri upatikanaji wa bidhaa muhimu na maisha ya wananchi.
Ameeleza kuwa kulinda amani ni jukumu la kila mwananchi, kwani utulivu wa jiji ni muhimu kwa kuendelea kwa biashara, usafirishaji, huduma na shughuli nyingine zinazotegemewa na wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi.

Hakuna maoni: