PEMBEJEO HAI KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI NA KUONGEZA TIJA YA KILIMO

DODOMA.

Serikali imewataka watafiti, wabunifu na wazalishaji wa pembejeo za kilimo ikolojia kuhakikisha bidhaa zao zinathibitishwa ubora na kusajiliwa kisheria ili kulinda wakulima, kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushindani wa mazao katika masoko ya ndani na nje ya nchi.


Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Pembejeo kutoka Wizara ya Kilimo, Samson Poneja, wakati akifungua Mkutano wa Kitaifa wa Wadau wa Pembejeo Hai za Kilimo Ikolojia Tanzania 2026, unaofanyika kwa siku mbili kuanzia Novemba 26 hadi 27 jijini Dodoma.


Mkutano huo umeandaliwa na Shirika la Iles de Paix (Island of Peace-IDP), kwa kushirikiana na Mtandao wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM) na wadau wengine, ukiwa na kaulimbiu isemayo “Kufungua fursa na kuimarisha uwezo wa matumizi ya pembejeo za kilimo ikolojia kutoka utafiti hadi matumizi kwa maendeleo ya sekta.”


Akizungumza katika mkutano huo, Poneja amesema mahitaji ya soko la dunia yamebadilika, huku wanunuzi wengi wakielekeza mahitaji yao katika mazao yanayozalishwa kwa kuzingatia misingi rafiki kwa mazingira na yasiyo na mabaki ya kemikali. Amesisitiza kuwa wakulima na wazalishaji wanapaswa kuanzia katika mahitaji ya soko kabla ya kupanga uzalishaji ili kuhakikisha mazao yanakidhi viwango vinavyohitajika.

Amesema sekta ya kilimo inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kupungua kwa rutuba ya udongo, ongezeko la visumbufu vya mimea, gharama za uzalishaji na uharibifu wa mazingira. Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kupitia sera, sheria na kanuni ili kuweka mazingira wezeshi kwa wadau, huku akihimiza ushirikiano kati ya taasisi za utafiti na udhibiti zikiwemo TARI na TOSCI, sekta binafsi na wakulima katika kufanikisha Mkakati wa Taifa wa Kilimo Ikolojia Hai wa mwaka 2030 na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TOAM, Dkt. Mwantima Juma, amesema upatikanaji wa viuatilifu mbadala ni mojawapo ya vipaumbele vya kimkakati vya kilimo hai, kutokana na wakulima wengi kukosa njia mbadala wanapohimizwa kuachana na matumizi ya viuatilifu vya kemikali. 

Amesema vijana wameonesha ubunifu mkubwa katika kutengeneza bidhaa mbalimbali, hivyo wanahitaji kuungwa mkono kupitia uwezeshaji, mwongozo wa usajili na gharama nafuu za ithibati.
Naye Mkurugenzi wa IDP, Ayesiga Buberwa, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wanasayansi na watafiti ili kukuza mifumo endelevu ya chakula na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo rafiki kwa mazingira. Amesema ubunifu wa kutengeneza mbolea na viuatilifu kwa kutumia malighafi za ndani kama korosho na katani unaonesha fursa kubwa kwa vijana, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mazingira yatakayowezesha bunifu hizo kukua na kuwafikia wakulima.

Akizungumza kuhusu mchango wa shirika hilo, Mkurugenzi wa Island of Peace Tanzania amesema mkutano huo unalenga kuunganisha nguvu za wadau wanaofanya kazi katika mnyororo mzima wa chakula, kuanzia uzalishaji hadi chakula kinapofika mezani. Amesema wanashirikiana na vyama na vikundi vya wakulima, asasi zisizo za kiserikali, sekta binafsi, watafiti na maafisa ugani kuanzia ngazi ya vijiji hadi wilaya ili kuimarisha mifumo endelevu ya chakula.

Ameeleza kuwa pembejeo hai, zikiwemo mbegu, mbolea, viuatilifu vya kudhibiti visumbufu vya mimea na zana za kilimo, zina mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji na kuhakikisha usalama wa chakula. Hata hivyo, amesema wazalishaji wengi wa viuatilifu hai, hususan vijana na wanawake, bado hawajasajiliwa kutokana na changamoto za gharama na taratibu za usajili.

Amesema mkutano huo unajadili fursa, changamoto na namna ya kupata ufumbuzi, kabla ya mapendekezo yatakayofikiwa kuwasilishwa katika majukwaa ya kikanda ya Afrika Mashariki. Pia amesisitiza umuhimu wa kuunganisha maarifa ya kisayansi na uzoefu wa wakulima ili kuhakikisha suluhisho zinazopatikana zinazingatia mazingira halisi ya jamii.

Changamoto za usajili na gharama za ithibati pia zimeibuliwa na wabunifu wanaojihusisha na uzalishaji wa mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini, wakieleza kuwa licha ya kuwepo kwa fursa kubwa, taratibu na gharama za udhibiti bado ni kikwazo kwa wajasiriamali wadogo.

Miongoni mwao ni kijana David Denis, ambaye ameeleza jinsi alivyobadili ndoto ya kuwa daktari na kujikita katika utafiti na uzalishaji wa mbolea kutokana na taka za nywele za binadamu. Amesema wazo hilo lilianza akiwa kidato cha tano na sita, baada ya kugundua kuwa nywele zilizokuwa zikitupwa au kuchomwa saluni zina virutubisho vinavyoweza kutumika katika uzalishaji wa mbolea.

Amesema utafiti wake ulionesha kuwa nywele za binadamu zina protini na kiwango kikubwa cha naitrojeni, hali iliyomshawishi kuanza kuchunguza namna ya kuzitumia kama malighafi ya kutengeneza mbolea. Alianza ubunifu huo kati ya mwaka 2017 na 2018 na kuendelea kuukuza hadi kuanzisha kampuni yake mwaka 2018.

Denis amesema alipochunguza soko la mbolea nchini alibaini kuwa kulikuwa na fursa kubwa ya uwekezaji, kutokana na utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje. Hata hivyo, amesema changamoto ya mitaji na gharama za taratibu za udhibiti zimekuwa vikwazo katika kukuza biashara hiyo, akitaja gharama ya dola za Marekani 10,000 kwa ajili ya kipimo cha ufanisi wa bidhaa (efficacy test) kuwa mzigo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.

Ameeleza kuwa uzalishaji wake umekua kutoka kiwanda kidogo hadi hatua ya kujenga kiwanda kikubwa eneo la Dakawa, mkoani Morogoro, chenye eneo la zaidi ya futi za mraba 1,000 na zaidi ya ekari 20 za eneo la mradi. Amesema wanatarajia kukamilisha kufunga laini ya uzalishaji ifikapo mwishoni mwa Januari, yenye uwezo wa kuzalisha lita milioni moja kwa mwaka na tani 100,000 za mbolea za aina ya Bulk.

Ametoa wito kwa Serikali kupitia upya sera, sheria na gharama za usajili na ithibati ili kuweka mazingira rafiki kwa vijana na wajasiriamali wadogo, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza bunifu za ndani na kupunguza utegemezi wa pembejeo kutoka nje.

Kwa upande mwingine, mtafiti wa mbolea asili, Mustapha Chonge, amesema amebaini matumizi ya mkojo wa ng'ombe kama pembejeo katika uzalishaji wa zao la alizeti yanaweza kuongeza tija kwa kiasi kikubwa, akieleza kuwa matokeo ya utafiti wake yameonesha uwezekano wa kuongeza uzalishaji hadi kufikia karibu mara mbili ya kiwango cha kawaida kwa ekari moja.

Chonge amesema ubunifu huo unaonesha namna rasilimali zinazopatikana katika mazingira ya wakulima zinavyoweza kutumika kama pembejeo mbadala, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza kipato cha wakulima.

Katika mkutano huo, wawakilishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) wameeleza umuhimu wa wazalishaji kuzingatia taratibu za kisheria, leseni, usajili na uthibitishaji wa ubora wa bidhaa kabla ya kuziingiza sokoni. Wamesisitiza kuwa hata viuatilifu hai vinahitaji kufanyiwa tathmini ya kisayansi ili kuhakikisha usalama wake kwa watumiaji, mimea na mazingira.

Naye Dkt. Angela Mkindi kutoka Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Arusha, amesema wadau wengi wa sekta hiyo hawajajumuishwa kikamilifu katika takwimu na mifumo ya taarifa iliyopo. Amehimiza kuwepo kwa mfumo mpana wa kuwabaini na kuwashirikisha wakulima, vikundi, vijana wabunifu, taasisi na kampuni ili kutambua mahitaji yao na kujenga ushirikiano wa muda mrefu.

Mkutano huo umehusisha mijadala ya kitaalamu, maonesho ya bidhaa na tafiti pamoja na kubadilishana uzoefu, huku mapendekezo na maazimio yatakayofikiwa yakitarajiwa kusaidia kuimarisha uzalishaji, usajili na upatikanaji wa pembejeo hai nchini na kuwasilishwa katika majukwaa ya wadau wa Afrika Mashariki.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.