TAMISEMI YAZITAKA HALMASHAURI KUTENGA FEDHA KUDHIBITI TAKA ZA PLASTIKI

DAR ES SALAAM

Halmashauri nne za Ilala, Temeke, Kinondoni na Mafia zimetakiwa kuhakikisha shughuli za udhibiti wa taka za plastiki zinapewa nafasi katika mipango na bajeti zao za kila mwaka ili kuwa na utekelezaji endelevu wa mikakati ya usimamizi wa mazingira.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Deogratius Mativila, wakati wa uzinduzi wa mipango ya kuboresha usimamizi wa taka za plastiki katika halmashauri hizo, ulioambatana na utoaji wa tuzo za Plastic Free Challenge.

Mativila amesema mafanikio ya udhibiti wa taka yanahitaji mifumo imara ya uratibu, usimamizi na uwajibikaji, huku halmashauri zikihakikisha miundombinu ya ukusanyaji na utunzaji taka inatunzwa na kuendeshwa kwa uendelevu. Amesema juhudi hizo zinaendana na msisitizo wa Serikali chini ya viongozi wakuu wa nchi kuhusu usafi wa mazingira na udhibiti wa taka za plastiki.

Amezitaka halmashauri kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wengine ili kupata fedha, teknolojia na utaalamu, huku elimu kwa wananchi kuhusu utenganishaji sahihi wa taka ikiendelea kutolewa. Amesisitiza kuwa masoko, vituo vya mabasi na maeneo ya biashara yanapaswa kupewa kipaumbele katika kuweka mifumo ya kutenganisha taka za plastiki, taka za kikaboni na aina nyingine ili ziweze kukusanywa na kuondolewa kwa wakati.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ForumCC, Justas Kibona, amesema ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na jamii ni muhimu katika kukabiliana na changamoto ya taka za plastiki. Amehimiza matumizi ya bidhaa zinazoweza kutumika tena, kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na urejeshaji taka pamoja na kusimamia wajibu wa wazalishaji kupitia mfumo wa Extended Producer Responsibility (EPR).
Katika tuzo za Plastic Free Challenge, Halmashauri ya Ilala imeibuka mshindi wa kwanza kupitia Soko la Kisutu, Soko la Buguruni na Stendi ya Mabasi ya Kinyerezi, na kujipatia Sh milioni sita.

Halmashauri ya Mafia, kupitia Soko la Mjinga, imeshika nafasi ya pili, huku Temeke kupitia Soko la Stereo ikishika nafasi ya tatu na Kinondoni kupitia Soko la Afrika Sana ikishika nafasi ya nne. Halmashauri hizo tatu zimepata Sh milioni nne kila moja.

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia amesema mipango endelevu ya usimamizi wa mazingira itasaidia kuifanya wilaya hiyo kuwa safi na salama, akieleza kuwa mazingira safi ya Mafia yanachangia pia katika kujenga Tanzania safi na kuwashukuru wadau walioshiriki katika juhudi hizo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.