Nkasi, Rukwa.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imeanza kutekeleza agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kuhusu ujenzi wa barabara ya kuelekea Kituo cha Afya cha Kasu yenye urefu wa mita 900 kwa kiwango cha lami.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake katika Jimbo la Nkasi Kusini aliyoifanya mwezi Machi, 2026 ambapo Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Moses Kayegele alipowasilisha ombi kwa Waziri Mkuu kuhusu kujengewa barabara hiyo kutokana na serikali kuwekeza fedha katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha mfano katika wilaya ya Nkasi.
Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Nkasi, Mhandisi Madirisha Lumala amesema changamoto kubwa iliyokuwepo katika Kituo hicho ni ukosefu wa barabara inayofikika kwa urahisi katika majira yote yaani wakati wa kiangazi na masika kutoka barabara kuu ya Sumbawanga-Mpanda.
Mhandisi Lumala amesema baada ya Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, Mhe. Moses Kayegele kuwasilisha ombi hilo Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa TARURA iangalie namna ya kujenga barabara hiyo kutoka barabara kubwa ya Sumbawanga-Mpanda yenye urefu wa takribani kilomita moja kwa kiwango cha lami.
"Baada ya maelekezo hayo TARURA tuliyapokea maelekezo na kuanza kufanya usanifu na kuwasilisha taarifa makao makuu na mara moja tukapewa kibali cha utekelezaji na mkataba umeanza rasmi tarehe 12 Oktoba, 2026 na tunatarajia mwezi Januari, 2027 tuweze kukamilisha kazi", amefafanua Mhandisi Lumala.
Bi. Margreti Chambo mkazi wa kijiji cha Kasu ameseme walikuwa wakipata changamoto hasa wakati wa masika ambapo mvua zikinyesha maji yalijaa hivyo kuwapa ugumu wa kufika kwa urahisi katika kituo hicho kupata huduma za afya.
Kwa upande wake, Bw. Filbert Tafilo ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji cha Kasu 'B' amesema eneo hilo lilikuwa na barabara ambayo ilikuwa haipitiki na kuongeza kuwa wakati wa masika wagonjwa kufika katika Kituo cha Afya ilikuwa ni shida na wakati mwingine wagonjwa walikuwa wanaanguka na bodaboda.
"Tunamshukuru Waziri Mkuu kwa kusikia kilio chetu sisi wananchi wa kijiji hiki lakini sio kijiji hiki tu ila kituo hiki kinahudumia takribani kata karibu sita maana yake ni kituo kikubwa", amesema
Amezitaja kata zinazohudumiwa na kituo hicho kuwa ni pamoja na kata za Kipande, Mkwamba, Nkandasi, Chala, Kate na Nyula na wanamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea adha hiyo.


Hakuna maoni: