Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan hii leo July 15,2023 amepokea Taarifa ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai hapa Tanzania, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt Samia Amesema kuna umuhinu mkubwa wa kushughulikia Mfumo wa Upelelezi ili kuondoa udhaifu wa ubobezi wa vyombo vinavyofanya upelelezi pia amesema ipo haja ya kufanya maboresho ya uendeshaji wa magereza nchini na kuyaweka katika hali nzuri.
"Uendeshaji wa magereza yetu nayo tukayatazame, hatusemi tuwe na magereza kama ya Ulaya chumba kila mtu chake, TV, hapana. Tutakwenda kwa uwezo wetu, lakini yawe magereza ambayo yanahifadhi watu.”
"Huu mfumo wa upelelezi na wenyewe tuushughulikie vizuri, lakini madhaifu mengine aliyotoa kwenye huo mfumo ni ubobezi kwa vyombo vyote vinavyofanya upelelezi, kidogo kuna udhaifu wa ubobezi na hili si kwa upande mmoja ni kwa pande zote mbili za muungano.”
"Mageuzi makubwa yanayotakiwa hapa ni sisi wenyewe kwanza alafu tunakwenda kiutawala, tunakwenda kwenye mambo ya kiufundi ambayo hayo sasa yanataka fedha, mengi yanataka fedha mengine tukifanya kazi kwa pamoja taasisi mbalimbali wala hayataki fedha nyingi."- Rais Samia Suluhu Hassan akipokea ripoti ya Tume ya Haki Jinai
Mwenyekiti wa Tume ya Haki Jinai, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande Wakati akiwasilisha Taarifa rasmi ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini, amesema Tume imebaini vyombo vyenye mamlaka ya ukamataji, mara kadhaa hutumia nguvu kupita kiasi na kusababisha mateso kwa watuhumiwa.
"Pili tumebaini uwepo wa Taasisi nyingi zenye Mamlaka ya kukamata zilizoidhinishiwa kuwa na Mahabusu na hii imesababisha ugumu kwa Wananchi kutambua Taasisi ipi inamuhifadhi Mahabusu Ndugu yao kibaya zaidi Mahabusu nyingine hazijulikani zilipo"
"Tume inapendekeza Taasisi nyingine zenye Mamlaka ya ukamataji zitekeleze ukamataji zikishirikiana pamoja na Jeshi la Polisi na sio Taasisi hizo pekee na pia Mahabusu za Jeshi la Polisi ndio pekee zitumike kuhifadhi Watuhumiwa wenye makosa ya jinai waliokamatwa"
"Tume tunapendekeza Mamlaka ya Kipolisi ya kukamata na kuweka mtu kizuizini waliyonayo Wakurugenzi na maafisa watendaji kata, yaondolewe kwao na jukumu hilo liachwe mikononi polisi”
“Tume tunapendekeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya wazingatie wanapotekeleza mamlaka ya ukamataji ni muhimu kufuata matakwa ya sheria, tunapendeleza Kiongozi anayekiuka maagizo awajibishwe na Serikali kwasababu kuna shauri linalotokana na DC wa Siha kumuweka Mshtakiwa ndani kwa makosa ya madai na Serikali ikawajbika kulipa Milioni 90” - Amesema Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande.




Hakuna maoni: