Na Emmanuel Kawau,
Dar es salaam.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamadi Masauni amesema ili kukabiliana na vitendo vinavyokinzana na Sheria ya usalama katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka 2023 wamejipanga kuongeza Askari na Operesheni maalumu barabarani pamoja na kuimarisha maeneo ya ukaguzi na kuondoa magari mabovu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam mara baada ya kikao kazi kilicholenga kujadili na kuweka mikakati mahususi ya muda mfupi na mrefu ya kuboresha ulinzi na usalama barabarani kati yake na Baraza la usalama barabarani.
Masauni amesema kuwa wamekubaliana kutumia njia za kisasa za ukaguzi wa magari ikiwa ni pamoja na kununua mashine na vifaa vyenye teknolojia ya kisasa za ukaguzi na kuweza kurahisha utendaji kazi na kupunguza msongamano unaopelekea magari kutumia muda mrefu.
Pamoja na hayo amewataka madereva na watumiaji wa barabara kufuata sheria za usalama barabarani bila shuruti.
Kwa upande wake Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani SACP Ramadhan Ng'anzi ametoa taarifa ya ajali,majeruhi na vifo vilivyotokea katika kipindi cha January hadi December 12/2023 ambapo jumla ya ajali zilizotokea ni 1,641 ambapo kati ya hizo ajali 1,057 zilisababisha vifo,ajali 451 zilisababisha majeruhi na ajali 135 zilisababisha uharibufu wa vyombo vya moto.
"Katika ajali hizo zilisababisha vifo kwa watu 1,550,kati ya vifo hivyo wanaume ni 1,189 na wanawake walikuwa 361.Aidha jumla ya majeruhi katika kipindi hicho ni watu 2,562 kati yao hao wanaume ni 1,721 na wanawake ni 841". Amesema Kamanda Nga'nzi.
Aidha amesema kuwa jumla ya madereva 1,226 wamefikishwa mahakamani huku madereva 2,596 wamefungiwa leseni zao kwa makosa mbalimbali.




Hakuna maoni: