PROF. KITILA MKUMBO ASHTUSHWA KASI YA MTO GIDE KUMOMONYOA UDONGO NA KUANGUSHA MAKAZI

 



Na Mwandishi Wetu,

Dar es salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali itachukua hatua madhubuti kuzuia mmomonyoko wa udongo unaokula makazi kutokana na kuhama kwa mito mkoani Dar es Salaam.

Profesa Mkumbo ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (CCM) alishuhudia hayo akiwa ziarani katika Kata ya Ubungo Dar es Salaam ambapo alijionea athari za mafuriko kwenye Mto Gide na kushuhudia baadhi ya makazi yakiwa yamesombwa na maji huku nyumba nyingine zikiwa hatarini ikiwemo moja ya majengo katika Hoteli maarufu ya Land Mark.

"Huu mmomonyoko namna unavyokwenda kwa kasi unatishia kutoweka kwa makazi mengi na hili jambo ni kubwa kuliko unavyoweza kufikiria, ipo haja ya kuchukua hatua kubwa zaidi" alisema Profesa Mkumbo.

Alisema namna athari zilivyo kwa mvua hizi za El-nino ni dhahiri kunapaswa kuwepo na hatua za dharula, muda mfupi, mrefu na wa Kati kwakuwa maji yanakuja kwa kasi kubwa.

Katika ziara hiyo Profesa Mkumbo alitembelea kivuko kinachotenganisha wakazi wa Ubungo Kisiwani na Ubungo Maziwa ambacho kimesombwa na maji na kuchukua hatua za dharula za kutafuta fedha kwaajili ya kujenga kivuko hicho kabla ya shule kufunguliwa January, 2024 ili kuwezesha wanafunzi na wananchi kupita bila shida.

Aidha waziri huyo amewaagiza TARURA kufanya tathimini ya haraka na kuanza ujenzi mara watakapokabidhiwa fedha kiasi cha Sh. Milioni 90 kinachotakiwa kukamilisha ujenzi huo.

Katika hatua nyingine, waziri huyo ameahidi kufanyiwa matengenezo ya dharula kwa baadhi ya barabara zilizoharibiwa na mvua pamoja na Vivuko huku akiwataka wananchi kuwa na subra wakati Serikali ikishughulikia changamoto zinazowakabili.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.