DKT BITEKO AWAPONGEZA WASANII KUUNZI UTAMADUNI WA KITANZANIA. AWATAKA KUENDELEA KUONESHA KWENYE KAZI ZAO ZA SANAA.
Na Emmanuel Kawau,
Dar es salaam.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko Amesema kuwa, wasanii wanao wajibu mkubwa wa kulifanya Taifa kuwa hai na kuthaminiwa na mataifa mengine kwa kuenzi tamaduni,mila njema, lugha Adhimu ya Kiswahili na tamaduni zinazolifanya taifa kuwa la kipekee Duniani.
Dkt. Biteko amesema hayo leo tarehe 29 Februari 2024 wakati akimwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa mwaka wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa uliofanyika jijini Dar es Salaam uliohudhuriwa na wasanii pamoja na wadau mbalimbali wa Mfuko huo.
Dkt. Biteko amewasifu wasanii nchini kwa kukataa kupuuza utamaduni wa Taifa na kuamua kwa pamoja kuupa heshima utamaduni huo kupitia kazi zao za sanaa hali inayofanya Taifa kujivunia.
“Kupitia kazi za sanaa lazima tuoneshe kuupenda utamaduni wetu na kuuishi na tunataka utamaduni huo uende mpaka nje ya mipaka ya nchi, kwani Taifa lisilo na utamaduni ni Taifa mfu hivyo tuuenzi utamaduni wetu ambao ni mzuri.” Amesema Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa, kwa miaka mingi kazi ya Sanaa ilikuwa ni kuelimisha na kuburudisha lakini sasa imepanuka na imekuwa ni nyenzo ya kutengeneza ajira na ndio maana Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua kufufua mfuko huo ambao ulianzishwa mwaka 1992 ambao ulikuwa ukisuasua lakini sasa umeimarika.
Dkt.Biteko amepongeza wasanii wote ambao wamekuwa wakizingatia vigezo na mashati ya kukopa na kurejesha mikopo kwa wakati na hivyo kuwataka wasanii kuhimizana juu ya umuhimu wa kukopa na kurejesha mikopo ili iweze kuwanufaisha wengine.
Amesema pamoja na ukweli kwamba Sekta ya Utamaduni na Sanaa inaongoza kwa ukuaji kati ya sekta zote nchini ikikua kwa asilimia 19 lakini bado mchango wake kwa pato la Taifa ni duni kwani inachangia asilimia 0.3 na hii ikimaanisha kuwa Sekta inakua lakini haichangii zaidi.
Amesema kuwa, Kupitia mfuko huo wataanzisha sehemu ya kutoa mafunzo maalum kwa wasanii wachanga na kuwanoa na kuwawezesha kuunda taasisi ambayo itakua na itakubalika kwenye benki ili kupata mikopo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Abdulmajid Nsekela alisema kuwa, mfuko huo unatoa huduma kuu tatu ambazo ni mikopo ya masharti nafuu kwa walengwa katika Sekta, kuwajengea uwezo wasanii kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ujasiriamali, urasimishaji, nidhamu ya biashara na kuwapa nafasi ya kuona fursa mpya zilizopo kwenye Sekta.
Ameongeza kuwa, katika siku za usoni mfuko unalenga kutoa ruzuku ili kuwawezesha wajasirimali katika Sekta hiyo.




Hakuna maoni: