MAZINGIRA WEZESHI KUIBEBA SEKTA BINAFSI.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Dkt. Godwill Wanga (kushoto) akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (katikati) mara baada ya kikao cha Kamati Tendaji cha TNBC kumalizika jana Ikulu jijini Dar es Salaam. (Kulia) ni Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo.

Na Mwandishi Wetu.

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan imesema itaendelea kuweka mazingira rafiki ya kufanya biashara pamoja na kuweka sera na sheria zitakazo wezesha sekta za umma na binafsi kushirikiana kuleta maendeleo kwa taifa.

Akizungumza kwenye kikao cha Kamati Tendaji cha Balaza la Taifa la Biashara (TNBC) jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera and Uratibu), Dk Jim Yonazi amesema serikali imejizatiti kuboresha mazingira ili kuvutia zaidi wawekezaji na wafanyabiashara sekta binafsi lengo likiwa kuinua ucchumi na kuongeza pato la Taifa.

“Tumekuwa tukirekebisha sera za nchi, sheria za kodi na sheria za usajili wa makampuni haya yote yote yanalenga kuweka mazingira bora ya kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini.” Amesema Dk Yonazi ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Balozi, Dk Moses Kusiluka.

Dk Yonazi alisisitiza kuwa serikali inaendeleza juhudi zake pia za kuhakikisha inasogeza huduma muhimu na stahiki kwa wananchi ili kuhakikisha mazingira ya ufanyaji kazi yanakuwa na tija kwa jamii

Naye Katibu Mtendaji wa TNBC, Dk Goodwill Wanga amesema kuwa kupitia vikao na mikutano ya baraza wamefanikiwa kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) ukitekelezwa kwa asilimia kubwa.

“Tunaona serikali inaendeleza juhudi na jitahida za kuhakikisha Watanzania wote wanafurahia huduma zinazotolewa na serikali ikiwa ni pamoja na kusomana kwa mifumo ili wanachi wapate huduma stahiki na kwa wakati,” amesema Dkt. Wanga.

Dk Wanga amesema serikali inaendelea kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vya kiutendaji, kutunga sheria na sera rafiki kwa wafanyabiashara pia kutafuta fursa za masoko makubwa ya kibiashara nje ya mipaka ya nchi.

Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu (BoT), Emmanuel Tutuba amesema kuwa sekta ya fedha imendelea kuimarika na kutoa mchango stahiki kwa sekta za umma na binafsi kwa kuhakikisha zinakuwa na ufanisi mkubwa na wenye tija kwa pato la Taifa.

“Tunapenda kuona wananchi wakichangamkia fursa ambazo kama Benki Kuu tunazitoa ikiwa pamoja na utoaji wa mikopo nafuu ambayo itasaidia kuleta ustahimilivu wa mitaji na miradi wanayoiendesha.”amesema GavanaTutuba 

Naye Mwenyekiti wa Kongani ya Madini kutoka sekta binafsi, Simon Shayo amesema kuwa kama sekta binafsi wanajivunia kuona kuwa serikali inaweka juhudi katika kutatua hoja ambazo zinaibuliwa na wafanyabiashara lakini pia kuongezeka kwa ubia na mjadala chanya kati ya serikali na sekta binafsi.

“Wito wetu kwa serikali ni kuwaomba waendelee kufanyia kazi changamoto na mapendekezo yote yanayotolewa na sekta binafsi na wafanyabiashara kwa ujumla kwa ujumla wake,” amesema Shayo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda, Biashara na Kilimo Tanzania (TCCIA), Oscar Kisanga amesema kuwa serikali imekuwa ikiwashirikisha kwa ukaribu sekta binafsi katika kujadili changamoto mbalimbali zinazo wakumba katika utendaji na kuwasaidia utatuzi wake.

“Tunaahidi kuendelea kutoa mchango na ushirikiano wetu wa karibu kwa serikali katika kuhakikisha juhudi zinazofanyika zinazaa matunda na kufikia hatima tunayoikusudia," amesema Kisanga.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Athuman Ngenya (kushoto) mara baada ya kikao cha Kamati Tendaji cha TNBC kumalizika jana Ikulu jijini Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.