WIZARA TATU KUJADILI,TALAKA,VIFO.





Na Mwandishi Wetu, 

Dodoma

WAZIRI wa Katiba na Sheria Balozi Dk Pindi Chana amesema amepanga kukutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutafuta suluhisho la ongezeko la vifo na wimbi la talaka katika jamii.


Kwa mujibu wa taarifa ya takwimu ya matukio muhimu ya binadamu ya Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), takwimu inaonesha kumekuwa na ongezeko la vifo kwa wanaume vinavyosababishwa na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza jambo ambalo linasababisha ongezeko la watoto waishio kwenye mazingira yasiyo bora kutokana na kukosa malezi ya pande zote mbili.


Aidha Waziri Chana amesema kwa upande wa hali ya ndoa, takwimu inaonesha ongezeko la usajili wa talaka limekuwa kubwa kwa kila mwaka jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa ukatili kwa watoto kwa kukosa malezi ya wazazi wawili.


Akizindua taarifa ya takwimu ya matukio muhimu ya binadamu pamoja na kufungua mafunzo ya uendelevu wa usajili wa watoto ya RITA mkoani Dodoma jana, Waziri Chana amesema katika takwimu za sensa kuhusu hali ya ndoa kwa mwaka huu RITA wamesajili talaka 800 ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambayo ilikuwa ni chini ya hapo hivyo ni wajibu wa Serikali kukaa na kuona wananusuru hali hii.


“Nahitaji kikao na Waziri wa Mambo ya Ndani ili tukae tuzungumze, takwimu za ajali, vifo kama tulivyoambiwa na taarifa ya RITA, tunafanyaje, haraka sana nahitaji kikao na waziri mwenzangu dadaangu Ummy Mwalimu, lazima tushee hizi data ili tupate kujua tunafanyaje.” amesema Waziri Chana.


Pia alisema kama ikiwezekana zinapopatikana takwimu za talaka wakati mwingine ni vema zipatikane na sababu ya talaka hizo ili kuona wanazitafutia vipi suluhisho.


“Katika takwimu za sensa ambazo Mwenyekiti amezielezea vizuri ni kwamba, takwimu za ‘single mother’ (ndoa) na kama mlivyosema talaka, safari hii wamesajili talaka 800, takwimu zipo, sasa lazima tuone tunafanyaje? Amesema na kuongeza,


“Katika changamoto ya ukatili wa watoto ni pamoja na ‘single parent’ (ndoa), mtoto akienda kwa baba yuko peke yake, akienda kwa mama yuko peke yake, anakosa ushirikiano. Hasa hili la ‘single parent’ kama ni sababu za ukatili kwa watoto, watoto hawa tunaojadili ndio kizazi cha viongozi wetu, akina Pindi Chana wanaokuja, tunahitaji sana kuwajali.” amesema.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA, Dk Amina Msengwa amemuhakikishia waziri Chana kuwa mpaka kufikia mwaka 2025 Wakala itahakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka 5 watakuwa wamesajiliwa ikiwa ni agizo kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.


Dk Msengwa amesema wao kama washauri wataendelea kuisimamia RITA na majukumu yake ipasavyo lakini kubwa ni kuhakikisha kwamba usajili unafikia malengo ambayo walikabidhiwa siku bodi yake inaingia kutekeleza majukumu yake.


“Mwaka 2025 tunategemea kwamba watoto wote chini ya miaka mitano tuwe tumewasajili, kwa hiyo tuwe tunawaona kwenye kanzidata zetu. Na pia ifikapo 2030 maana yake tunategemea wananchi wote tuwe tumewasajili.” Amesisitiza Mwenyekiti huyo.


Naye Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi amesema kumekuwa na matokeo chanya ya usajili wa matukio ya binadamu kutokana na juhudi zinazofanywa na serikali na wadau sababu zinazochangia kupatikana kwa mafanikio mbalimbali nchini.


Kanyusi amesema ni pamoja na utekelezwaji wa mikakati, programu na kampeni za usajili, kuongeza viwango vya upatikanaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kutumia mifumo ya Tehama katika kusajili watoto.


“Wakala tunaahidi kuendelea kusimamia program zilioanzishwa ili kuhakikisha zinakuwa endelevu na wananchi wanawezeshwa kusajili matukio haya mara yanapotokea,” emesema na kuongeza,


Tunaendelea kubuni mikakati kwa ajili ya kuwezesha kupatikana kwa mafanikio zaidi ili katika ripoti inayofuata tuwe na matokeo bora zaidi ya haya.” amesisitiza Kanyusi.


Wakizungumza katika uzinduzi huo wadau wa maendeleo na usajili kutoka mashirika ya kimaendeleo waliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wakala hao katika masuala mbalimbali muhimu ikiwemo kuhakikisha watoto wote wanasajiliwa na kuhakikisha upatikanaji sahihi wa takwimu zitakazowezesha kupanga mipango mbalimbali ya nchi.


Uzinduzi wa taarifa ya matukio muhimu ya binadamu na ufunguzi wa mfumo endelevu wa usajili wa watoto na kikao kazi kuhusu uendelevu wa usajili wa watoto katika vituo tiba na ofisi za kata imehusisha maofisa usajili kutoka mikoa mbalimbali nchini, wadau wa maendeleo pamoja na maofisa waandamizi kutoka wizara na taasisi za Serikali.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.