BOT YAJA NA MPANGO WA KUPUNGUZA GHARAMA ZA KUTUMA FEDHA MTANDAONI.


Na Mwandishi wetu,

Dar  es Salaam

Katika jitihada ya kuwawezesha Watanzania maskini kushiriki katika ujenzi wa Taifa na kunufaika na uchumi wa kijiditali, Benki Kuu ya Tanzania imebuni mpango wa kutuma fedha mtandaoni ambao gharama zake zitakuwa chini ya zile zinazotozwa na kampuni za simu nchini na wadau wengine.

Gavana wa Benki Kuu (BoT), Bw Emmanuel Tutuba, ameeleza kuwepo kwa mpango huo wakati akiongea na waandishi wa habari ambao walitaka aeleze kidogo umuhimu wa Mpango Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali Tanzania wa miaka 10 (Tanzania Digital Economy Strategic Framework 2024-2034). Alisema Benki Kuu hivi karibuni imezindua mpango ambao ni rahisi kwa mtu kutoa fedha kutoka akaunti yake, akapitisha fedha hiyo katika mpango huo unaoitwa TIPS (Tanzania Instant Payment System) ambao umeunganisha wadau mbali mbali ili malipo yafanyike kwa urahisi; yaani mtu kutokea benki yake aweze kumlipa mtu kwenye benki nyingine au kampuni ya simu.


Alieleza kuwa kwa kupitia TIPS mtu atatumia mpango huo kulipa kodi na kulipia huduma nyingine.


Kuhusu mpango mkakati Bw Tutuma, alisema mpango huo unawahimiza na kuwawezesha wadau mbali mbali kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kutumia mifumo ya Benki Kuu.


“Na kuzinduliwa kwa mpango huu, sisi tunaona hii ni hatua kubwa sana. Sisi kama wadhibiti wa masuala ya mifumo na malipo hapa nchini mpango huu utaharakisha kufikisha fedha kwa walengwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na kufika salama ili fedha hiyo isaidie kuinua shughuli za kiuchumi,” alisema.


Aliwahakikishia Watanzania kwamba Benki Kuu wakati wote inahakikisha mitandao ya Tanzania ni salama. “Sisi kama BoT tunachukua hatua mbali mbali kuwalinda wateja. Nachukua fursa hii kuwatoa hofu watumiao mifumo kwa malipo. Tumeweka misingi mizuri ya kufikisha fedha kwa walengwa,” alisisitiza na kufafanua kwamba benki kuu ina kitengo cha kulinda mteja na pia gavana ni mwenyekiti kamati ya kudumu ya usalama mitandaoni (cyber security steering committee). Vyombo vyote vinalenga kumlinda mteja.


Gavana Tutuba alieleza kuwa katika kukuza na ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali, benki itatekeleza mipango mizuri kwa awamu. Alisema siku za usoni watu watatumia cheki zinazosomwa na mifumo ya Tanzania kote nchini. Baadaye Watanzania watatumiwa codebars katika malipo na awamu itakayofuata benki itatengeneza “kadi maalumu kufanya malipo hata kama mtu yupo offline kwa gharama ndogo sana.”


Amewaomba Watanzania na wadau wengine waendelee kutimia mifumo ya kidijitali iliyopo na kusisitiza kuwa: “Sisi BoT tutaendelea kuisimamia mifumo iliyopo, iko vizuri, na mifumo hiyo inasomana na BoT.”

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.