Na Mwandishi Wetu,
Kushoto,Tanga
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Lushoto, OCD Omary Mshangama, amewaonya vijana wanaojihusisha na vikundi vya uhalifu katika Kata ya Magamba mkoani Tanga kuacha mara moja kabla hatua kali za kisheria hazijachukuliwa.
Kamanda huyo alitoa onyo hilo wakati alipopata taarifa kuwepo na baadhi ya matukio yasiyofaa kutokana na tukio la hivi karibuni la baadhi ya vijana kutaka kuwadhuru timu ya wataalamu wa utafiti za viumbe hai (baionowai) walikuwa wakiendeleza mchakato ulioanza mwaka 2022 wa tathmini ya athari za mazingira na kijamii.
"Hatutamvumilia yeyote yule awe kiongozi wa serikali anayeweka hili genge huku, ama mtu yeyote yule na hii siyo Magamba pekee yake, hili onyo ni kwa wilaya nzima," amesema.
Ikumbukwe hivi karibuni watafiti hao walikwenda kufanya utafiti maeneo ambayo serikali ilizuia uchimbaji wa madini kutokana na athari za mazingira kwa wananchi,
Kamanda wa polisi aliwataka wananchi kutochukua sheria mkononi badala yake, wanapaswa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na jeshi la polisi litachukua hatua kali dhidi ya wale wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.
"Wakija watu mjue wameshapita ngazi za serikali hivyo ni muhimu kupewa ushirikiano wa kina siyo kuwashikia mapanga na kutaka kuwadhuru sitokubali hali hii iendelee, kama jeshi la polisi tunatoa onyo kwanzia sasa yeyote atakayebainika kujihusisha na matukio ya kiuharifu toeni taarifa msifichane" amesema Mshangama.
Hata hivyo wakazi wa eneo la Mgodi wa Mawe ya Bauxite ambao serikali umeufungia kutokana na madai ya madhara kwa wananchi walielezea changamoto wanazokabiliana nazo, ikiwemo matumizi ya maji kutoka kwenye shimo lililofungwa.
Halima Hussein amesema kuwa wamekuwa wakitumia maji hayo kwa muda mrefu sana kwa matumizi ya kufua nguo hata kuoga na hawajawahi kupata madhara yoyote yale ya ngozi.
"Tunaiomba serikali kama inawezekana watafute wawekezaji wa eneo hili maana haya machimbo yakichimbwa na sisi tutapata ajira ambazo zitatujenga kiuchumi tusitegemee kilimo pekee tutapata shule nzuri na huduma za kijamii pia hata wilaya yetu itaingiza mapato makubwa ila kwa sasa wananchi wanapata wasiwasi" amesema Halima.
Hakuna maoni: