Na Mwandishi Wetu,
Dodoma.
MRADI wa Kijani Hai unaotekelezwa katika Mkoa wa Simiyu na Singida chini ya ufadhili wa Laudes Foundation ya nchini India na kutekelezwa na Giz na Helvetas Tanzania umewezesha zaidi ya wakulima 60,000 kulima Pamba kwa njia ya kilimo ikolojia hai.
Hayo yamesemwa na Meneja Mradi, Andrew Mphuru wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii katika maonesho ya Nane Nane yanayofanyika mkoani Dodoma.
Mphuru amesema mradi huo ambao umejikita katika kilimo cha pamba hai ulianza mwaka 2017, hadi sasa umefanikiwa kufikia zaidi ya wakulima 60,000 ambapo maratajio yao ni kufikia wakulima 100,000 kufikia mwaka 2028
Amesema mradi unashirikisha wadau wa pamba hai ambao ni Alliance Ginery, Bio Sustain, SM Holding na Remei ambapo lengo lao ni kuwaondoa wakulima kuachana na matumizi ya kemikali na kujikita katika kilimo endelevu.
“Mradi wa Kijani Hai ulianza mwaka 2017 na umefikia zaidi ya wakulima 60,000 ila lengo letu ni ifikapo 2028 tuwe tumefikia wakulima 100,000 na hekari 150,000 za pamba hai ziwe zinalimwa kwa njia ya kilimo ikolojia hai,” amesema.
Amesema matarajio yao hadi mwaka 2028 wawe wamerejeresha bioanuai katika hekari 150,0000 katika mikoa ya Simiyu na Singida.
Meneja huyo amesema ujio wa mradi huo wa kuhamasisha kilimo cha pamba hai umewezesha Tanzania kushika nafasi ya kwanza Afrika na tano Dunia kwa pamba bora.
Mphuru amesema Kijani Hai kwa kushirikiana wadau wengine watahakikisha kilimo hicho kinalimwa na kila mkulima.
Kwa upande wake Leonard Mtama anasema mradi huo umewezesha wakulima wa pamba nchini kuunganishwa na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mtama amesema uzalishaji wa pamba inayotokana na kilimo hai umeongezeka kutokana na elimu kwa wakulima kupitia maofisa ugani wao na wale wa serikali.
“Kupitia mradi wa Kijani Hai, tumehakikisha wakulima wanapata mafunzo na mbinu za kudhibiti wadudu waharibifu wa pamba na matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo. Lakini pia kampuni hizi za wanunuzi wa pamba hai zinawapatia bei zaidi (Premium) ya ile bei elekezi iliyotangazwa na serikali,” amesema.
Amesema takwimu zinaonesha tangu mwaka 2017 hadi sasa kuna ongezeko la asilimia 30 ya uzalishaji wa pamba mbegu, huku vitendo vya uchakachuaji vikipungua kama sio kuisha.
“Uchakachuaji wa kuweka maji, mchanga na vingine kwenye pamba umepungua kwani maofisa ugani wa kampuni na waserikalini wamekuwa wakifuatilia kuanzia shambani hadi sokoni,” amesema.
Naye Tawanda Mutonhori kutoka Kampuni ya Bio Sustain Ltd (T) ya mkoani Singida amesema kilimo ikolojia hai kimeweza kuongeza kiwango cha pamba bora katika mikoa ambayo wananunua.
“Sisi tunanunua pamba iliyolimwa kwa njia ya kilimo ikolojia hai kwa wakulima zaidi ya 24,000 wa mikoa ya Singida, Simiyu, na Shinyanga, kusema kweli pamba yao ni bora na inakubalika katika soko,” amesema.
Mutonhori amesema kampuni yao kwa mwaka inanua tani elfu 26 hadi 36 ya pamba iliyolimwa kwa njia ya kilimo hai, lakini lengo lango ni kununua tani elfu 50.
Amesema mikakati yao nikuanza kuchakata pamba katika kiwanda kipya kilichopo wilayani Meatu mkoani Simiyu ambacho kitakuwa kinahudumia wakulima wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mwakilishi wa Kampuni ya Alliance Ginery ya mkoani Simiyu, Masalu Samweli alisema kwa miaka mitatu wamewezesha zaidi ya wakulima 22,000, kulima pamba kwa njia ya kilimo hai.
Amesema Alliance Ginery ilianza kutoa elimu kuhusu faida za kilimo ikolojia hai kiafya, kimazingira na utunzaji wa ardhi, jambo ambalo limepokelewa vizuri.
“Kwa uzoefu wangu wa miaka mitatu ya kutoa elimu kuhusu kilimo ikilojia hai, uzalishaji wa mazao yasiyo na kemikali umeongezeka, hivyo wameweza kuona faida, hasa kupunguza gharama za uzalishaji, kutunza afya ya wakulima na ardhi na kurejeresha mazingira katika maeneo wanayohudimia,” amesema.
Masalu amesema pia Alliance Ginery imeweza kuongeza bei ya pamba (Premium) ambayo inazalishwa kwa njia ya kilimo ikolojia hai, hali ambayo imekuwa kivutio kwa wakulima wa zao hilo katika mikoa mbalimbali, kama Mwanza, Geita, Shinyanga, Tabora na Mara.
Ofisa huyo amesema pia kampuni hiyo imeweza kuwapatia wakulima molasesi ili kutega mitego ya kunasa wadudu waharibifu na kupanda mazao ambayo yanazuia wadudu kushambulia pamba. Pia alisema huwa wanawapatia viuatilifu vya asili kama ndulele, mwarubaini na vinginevyo.
“Wakati tunaingia kwenye zao la pamba wakulima walikuwa wanapata kilo 200 kwenye hekari moja, ila kilimo ikolojia hai kimeongeza mavuno hadi kufikia tani moja kwa hekari kwa baadhi ya wakulima.,” amesema.
Kwa upande wake Mkulima wa zao la Pamba wilayani Ikungi mkoani Singida, Solo Lameck amesema tangu kuanza kulima kwa mbinu za kilimo ikojojia hai ameweza kunufaika, hivyo kuitaka jamii kujikita huko.
“Kilimo hiki kinapunguza gharama kwa mkulima, hasa kwenye pembejeo, kama vile matumizi ya pumba za mbao na pamba yenyewe ambavyo hutumika kutengenezea makaa ya mimea ambayo inasaidia kuongeza rutuba kwenye ardhi. Lakini pia tumekuwa tukizingatia vipimo kwenye kilimo,” amesema.
Lameck amesema katika zao la pamba ambalo wanalima kwa njia ya kilimo ikolojia hai wanatumia kipimo cha sentimita 30/30 shina hadi shina na 60/60 mstari hadi mstari kimekuwa na matokeo kwa mkulima zaidi.
Amesema elimu ya kilimo ikolojia hai mkoani Singida imeweza kuongeza wazalishaji wa zao la pamba na wameweza kubadilika kiuchumi na kiafya.
Naye, Ofisa wa Uhifadhi na Bioanuai Emmanuel Lufilisha, alisema’ Mradi wa Kijani Hai umejikita pia katika utunzaji wa mazingira kupitia programu mbalimbali ambazo huanza na mafunzo kwa jamii na kisha kusimamia utekelezaji wake.
Lufilisha amesema programu hizo zimekuwa zikishirikisha wadau katika ngazi ya mkoa, wilaya, kata na vijiji.
Amesema kwa kushirikiana na baraza la halimashauri za vijiji, mradi huu umeweza kuunda kamati za mazingira za vijiji ambao ndio wasimamizi wakuu wa shughuli za uhifadhi wa mazingira.
“Hata hivyo, mradi huu umefanikiwa kuunda mtandao wa vijana ambao ni mabalozi wa mazingira, wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuhamasisha jamii juu ya uhifadhi wa mazingira na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Sambamba na hayo, mradi huu umekuwa mstari wa mbele katika kusimamia shughuli za urejeshaji wa uoto katika maeneo yaliyo haribiwa kwa njia ya upandaji miti na utunzaji wa visiki vilivyo hai kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kidini, afya na elimu,” amesema.
Hakuna maoni: