DCEA Yakamata Kilogramu 1,815 za Skanka na Watuhumiwa Watano Jijini Dar es Salaam.




DAR ES SALAAM.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya aina ya skanka kilichokadiriwa kuwa kilogramu 1,815 katika operesheni maalum iliyoendeshwa kuanzia tarehe 28 Agosti hadi 02 Septemba 2024. Operesheni hiyo ilifanyika katika maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni jijini Dar es Salaam, ambapo watuhumiwa watano walikamatwa kuhusiana na dawa hizo.


Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kufichua majina ya watuhumiwa. Richard Henry Mwanri (47), mfanyabiashara mkazi wa Mbezi Makonde wilaya ya Kinondoni, na Felista Henry Mwanri (70), mkulima mkazi wa Luguruni Mbezi wilaya ya Ubungo, ni miongoni mwa walioshikiliwa. Felista ni mmiliki wa nyumba ambapo dawa hizo zilipatikana.


Watuhumiwa wengine walikamatwa ni Athumani Koja Mohamed (58), mfanyabiashara kutoka Tanga, Omary Chande Mohamed (32), dereva bajaji kutoka Buza jijini Dar es Salaam, na Juma Abdallah Chapa (36), mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam. Katika operesheni hiyo, DCEA pia ilikamata gari aina ya Mitsubishi Pajero lenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV.


Kamishna Jenerali Lyimo alieleza kwamba Richard Mwanri ni mmoja wa walionekana kuwa na mtandao wa kuingiza dawa za kulevya nchini kwa kutumia magari huku akificha bidhaa hizo kwa kuchanganya na vitu vingine. Dawa hizi zina kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC), inayoweza kuathiri mfumo wa fahamu, akili, na kuleta matatizo kama vile magonjwa ya moyo, figo, na ini.


Kamishna Lyimo aliongeza kuwa matumizi ya skanka kwa wajawazito yanaweza kusababisha madhara kwa mtoto aliye tumboni, ikiwa ni pamoja na athari kwa maendeleo ya ubongo na uzito mdogo wa kuzaliwa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.