MALAWI WAJIFUNZA KUANZISHA SHIRIKA LA UCHIMBAJI MADINI KUPITIA STAMICO; _Waitaja Tanzania kuwa mfano wa kuigwa.




📍Dodoma

Katika jitihada za kuimarisha Sekta ya Madini nchini Malawi, Ujumbe wa Jamhuri ya Malawi pamoja na Sekretarieti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Uchimbaji na Madini nchini humo (MMRA) umefanya ziara rasmi nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza kutoka kwa Shirika la Madini la Taifa la Tanzania (STAMICO) ili kupata uzoefu wa kuanzisha Shirika la Uchimbaji Madini la Serikali ya Malawi.

Ujumbe huo ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini ya Malawi Martin Kaluluma Phiri, umejumuisha Wataalam wa madini na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Madini ya taifa hilo, waliokuwa na shauku ya kujifunza mbinu bora za kiutendaji.

Ujumbe huo upo nchini kwa ziara hiyo maalum ya kijifunza kutoka kwa STAMICO ambapo leo Septemba 13, 2024 wametembelea Ofisi za Wizara ya Madini Mtumba Jijini Dodoma na kufanya mazungumzo na Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga.

Akizungumzia ziara hiyo, Phiri amesema kuwa STAMICO ni shirika lenye uzoefu mkubwa katika kusimamia rasilimali za madini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, na kwamba wana shauku kubwa ya kujifunza mbinu bora za kiutendaji.

“Ziara yetu imejikita kwenye maeneo muhimu ya utendaji kazi wa STAMICO, ikiwemo uanzishaji wa shirika hilo, mifumo ya usimamizi wa rasilimali za madini, na mbinu za kuunganisha miradi ya uchimbaji madini kwa manufaa ya taifa” amesema Phiri.

Vilevile, Phiri amezishukuru Wizara ya Madini, STAMICO, na Serikali ya Tanzania kwa ukaribisho mzuri na kubainisha kuwa ziara hiyo imefungua fursa mpya kwa Malawi na kuwa wamejifunza mengi kuhusu jinsi ya kuunda shirika lenye nguvu na uwezo wa kusimamia rasilimali za madini kwa niaba ya wananchi huku akisisitiza kuwa Uzoefu wa Tanzania ni mfano mzuri wa kuigwa.

Aidha, ujumbe huo umepata fursa ya kujionea namna STAMICO inavyoshirikiana na Wawekezaji binafsi kupitia ubia wa kimkakati, hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia Sekta ya Madini.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, amesema kuwa mafanikio ya STAMICO yamejengwa kwa misingi ya ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi na kuongeza kuwa “Ni muhimu kuwa na uwazi katika usimamizi wa rasilimali za madini na kuhakikisha kunakuwa na utaratibu thabiti wa kufuatilia miradi ya uchimbaji,” amesisitiza Kamishna Mwanga.

Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Malawi kuboresha sekta yake ya madini kwa kuanzisha shirika la umma la uchimbaji madini litakalowezesha taifa hilo kupata faida zaidi kutokana na rasilimali zake, huku likinufaika na uzoefu wa nchi jirani kama Tanzania.

Viongozi wa pande zote mbili wameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuendeleza sekta ya madini kwa manufaa ya wananchi wa mataifa hayo

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.