MATOKEO YA ROYAL TOUR YAONEKANA MOYOWOSI, IDADI KUBWA YA WATALII NA MAPATO VYAONGEZEKA - DKT. FLORENCE SAMIZI (Mb)
Na. Beatus Maganja
Mbunge wa Jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo Mhe. Dkt. Florence Samizi amesema filamu maarufu ya Tanzania The Royal Tour iliyochezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta matokeo makubwa Katika Pori la Akiba Moyowosi linalosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini - TAWA wilayani humo kutokana na ongezeko kubwa la wageni wa uwindaji wa kitalii wanaotembelea hifadhi hiyo na kuiingizia Serikali mapato makubwa.
Dkt. Florence ameyasema hayo Septemba 27, 2024 wakati wa ziara ya mafunzo kwa ajili ya madiwani wa Halmashauri ya Kibondo, Kamati ya siasa ya Kibondo (W) na Sekretarieti ya Kibondo (W) ikiwa na lengo la kuwawezesha kuona jitihada zinazofanywa na Serikali katika kusimamia rasilimali za wanyamapori pamoja na uendelezaji wa shughuli za uhifadhi hifadhini humo Kwa kuzingatia ilani ya CCM. Ziara iliyoratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kusimamiwa na TAWA.
Mbunge huyo amesema kutokana na jitihada za Mhe. Rais Samia kutangaza utalii wa nchi yetu na kuupa kipaumbele hifadhi ya Moyowosi imetia fora mwaka huu Kwa kupata idadi kubwa ya wageni wa uwindaji wa kitalii na ongezeko kubwa la mapato.
"Hii Hifadhi ya Moyowosi imekuwepo miaka mingi lakini ilikuwa haijafanya vizuri Kwa kutia fora kama ilivyofanya mwaka huu (2024)" amesema Dkt. Florence
"Tumepata taarifa kwamba Mwaka 2022/23 walipata wageni 39 tu lakini mwaka huu wamepata wageni 89 mara 3 ya wageni waliopata mwaka uliopita lakini pia mapato yameongezeka ambapo mwaka 2022/23 hifadhi ilipata mapato ya bilioni 2.4 kwa mwaka. Lakini leo tunapoongea hata mwaka haujaisha tayari hifadhi imeshakusanya bilioni 3 kutokana na shughuli za uwindaji wa kitalii" ameongeza
Samizi amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Kwa Kazi kubwa aliyoifanya ambayo imepelekea ongezeko kubwa la watalii nchini na kusisitiza si watalii wa utalii wa picha pekee bali hata watalii wa uwindaji wa kitalii nao wameongezeka na kupelekea jamii zinazozunguka hifadhi ya Moyowosi kunufaika kwa mapato hayo.
Akizungumzia namna jamii inayozunguka hifadhi hiyo inavyofaika na shughuli za utalii, Mhe. Dkt. Florence amesema Kwa kipindi cha mwaka 2024 vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo tayari vimeshapokea shilingi Milioni 89 ambazo zimetumika Katika kuibua miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi wa madarasa, ujenzi wa ofisi za Serikali za vijiji, madawati pamoja na ununuzi wa viti vya watu wenye ulemavu
Awali akitoa maelezo kuhusu Hifadhi ya Moyowosi Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Kanda ya Magharibi Wilbright Munuo amesemea Hifadhi ya Moyowosi imekuwa na faida kubwa kwa vijiji jirani vinavyoizunguka kutokana na mapato makubwa inayoiingizia Serikali ambayo Kwa asilimia kubwa yanarudi kwa jamii.
"Sote tumeona kwamba Hifadhi hii ina faida kubwa, kwa mwaka tu wa fedha uliopita imekusanya zaidi ya bilioni 3, lakini pia zaidi ya milioni 134 zimeenda pia kwenye Halmashauri ya Kibondo ikiwemo zaidi ya millioni 89 ambazo zimetokana na ada ya wanyamapori lakini zaidi ya millioni 45 ambazo zimetokana na dola 5,000 ambazo zinalipwa kutoka Katika kila kitalu cha uwindaji kinawindisha Katika Pori la Akiba Moyowosi.
Munuo ameongeza kusema kuwa Katika jitihada za kuongeza mapato ya Hifadhi hiyo, Moyowosi imekuwa miongoni mwa hifadhi zilizoingizwa Katika mpango wa biashara ya hewa ukaa.
Aidha ametoa wito Kwa washiriki wa ziara hiyo kupeleka ujumbe kwa jamii kuacha vitendo vya uhalifu Katika hifadhi hiyo ikiwemo kuchungia mifugo, uharibifu wa mimea, ujangili wa wanyamapori pamoja na uvuvi haramu huku wakiwasisitiza kuunga mkono jitihada za Serikali katika shughuli za uhifadhi na uendelezaji wa shughuli za utalii sambamba na kutekeleza kwa vitendo ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Hakuna maoni: