Kahama, Shinyanga.
Wanawake nchini wamehimizwa kuendelea kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya madini ikiwemo kuwekeza kwenye shughuli za uchimbaji pamoja na kutoa huduma migodini kwa kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa kila mtu kushiriki katika uchumi wa madini bila kujali jinsi yake kwa kuzingatia Sheria na taratibu zinazotakiwa kufuatwa.
Wito huo ulitolewa Mjini Kahama na Mchimbaji Mdogo Mwanamama Asha Hassan Msangi maarufu kama Mama Nakio wakati akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini baada ya kutembelea shughuli za uchimbaji mdogo wa madini Wlayani Khama Mkoa wa Shinyanga.
Mama huyo aliyejizolea umaarufu mkubwa katika uchimbaji wa madini pia ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Manda Gold Mine alitoa wito kwa kina mama na wanawake kwa ujumla kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya madini huku akitolea mfano hai wa mafanikio yeke binafsi kupitia safari ya kihistoria hadi kuingia katika shughuli za uchimbaji madini na hatimaye kujizolea umaarufu mkubwa Mjini Kahama.
Mama Nakio, ambaye hivisasa anamiliki leseni 12 za uchimbaji mdogo wa madini (PML), alianza safari yake ya kibiashara katika kilimo cha mpunga. Hata hivyo, kutokana na azma yake ya kufanikiwa zaidi, aliamua kuingia kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, hatua ambayo imebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza kuhusu safari yake, Mama Nakio ameeleza kuwa baada ya kufanya biashara ya mpunga na mchele, ilimchukua muda kidogo kufanikiwa katika shughuli zake za uchimbaji kupitia msaada wa Serikali katika kumpatia umiliki wa leseni za uchimbaji, “Kwa msaada wa Serikali, niliweza kupata leseni, jambo ambalo limenifungulia milango zaidi kwenye sekta hii ya madini,” amesema Mama Nakio, akiongeza kuwa wanawake wanayo nafasi kubwa katika kuchangia mnyororo wa thamani kwenye sekta hiyo kama ilivyo kwake.
Mama Nakio alisema kuwa, wanawake wanayo nafasi kubwa ya kubadili maisha yao kupitia sekta ya madini, huku serikali ikiendelea kuwaunga mkono kwa kuwapa fursa za kupata leseni na elimu ya uchimbaji. “Wanawake wanayo nafasi kubwa katika sekta ya madini, siyo tu kama wachimbaji bali katika mnyororo mzima wa thamani, kuanzia uchimbaji hadi usindikaji, ukiangalia hapa hapa utagundua kuwa wanawake wengi ndio wanaoongoza kutoa bei nzuri katika ununuzi wa mawe haya kabla ya kwenda kwenye krasha, na baada ya kufanya taratibu zote wanajipatia vipato vizuri tu vinavyokimu maisha yao na familia zao, pia wao ndio wanaotoa huduma za vyakula kwenye maeneo ya wachimbaji” alisisitiza Mama Nakio
Aidha, Mama Nakio aliishukuru Serikali kwa Kuweka Mazingira wezeshi kwa watu wote kushiriki kwenye uchumi wa madini hatimaye kufanikisha ndoto zao na kubadilisha maisha yao na jamii kwa ujumla, “Kipekee tunamshuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mama ametuinua sana wanawake katika kipindi hiki cha uongozi wake, tunaishukuru pia Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini, kwa kweli huyu Afisa Madini Mkazi wa hapa (Kahama) ni mwanamama mwenzetu mchapakazi na msikivu sana, anatufanya wanawake tujivunie” alisisitiza Mama Nakio.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Winnifrida Mrema kupitia uzoefu wake, alieleza ugumu uliokuwepo kwa wanawake kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini moja kwa moja tofauti na kipindi cha sasa kwani Serikali imeweka mazingira wezeshi na rafiki kwa kila mtu kushiriki katika uchumi wa madini bila kujali jinsi yake.
“Nakumbuka wakati sisi tunaingia katika shughuli hizi za sekta ya madini, tulipokuwa tukienda kwenye shughuli za ukaguzi migodini kuna baadhi ya watu nwalikuwa wanatushangaa, lakini sasahivi idadi ya wanawake imekuwa kubwa sana katika mnyororo mzima wa shughuli za madini, kuanzia uchimbaji wenyewe, uchenjuaji na biashara ya madini, hadi watoa huduma migodini” alisisitza Mrema.
Aidha, Afisa madini huyo alimpongeza Mama Nakio kwa juhudi zake, akisema kuwa ni mfano wa kuigwa na wanawake wengine nchini na kuongeza “mfano mzuri tunao hapa Kahama, huyo Mama Nakio ameonyesha kuwa inawezekana, amejikita katika sekta hii na sasa anaendelea kufanya vizuri, kwa kweli tunawaomba wanawake wengine wajitokeze kwa wingi na kuchangamkia fursa hizi,” alisema Mrema.
Sambamba na hilo, Winnifrida Mrema alitoa rai kwa watu wote wenye leseni mbalimbali za kimadini, hususan wanawake kuzifanyiakazi leseni hizo kwa kuzingatia Sheria ya Madini na hivyo kuweza kujiimarisha kiuchumi.
Sekta ya madini imekuwa ni nguzo muhimu katika uchumi wa Tanzania, na kwa kuhusisha wanawake, inawezekana kuongeza kasi ya ukuaji na maendeleo endelevu. Kupitia ushuhuda wa Mama Nakio ameonyesha kuwa, kwa kujituma na kujiamini, wanawake wanaweza kufikia mafanikio makubwa katika sekta ambazo hapo awali zilionekana kuwa za wanaume pekee.
Serikali kupitia Wizara ya Madini iko mbioni kuzindua Programu ya Uchimbaji kwa Kesho Bora (Mining for a Brighter Tomorrow – MBT) yenye lengo la kuwajengea uwezo makundi ya kina mama na vijana wanaojishughulisha na shughuli za Uchimbaji wa Madini pamoja na mnyororo mzima wa Sekta ya Madini nchini. MBT itawasaidia Wanawake na Vijana kwa kuwaendeleza au kuwainua kwa kuwapatia leseni za maeneo ya kuchimba, magari, vifaa na mitambo ya uchorongaji.
Hakuna maoni: