Dhana ya Madini ni Maisha na Utajiri imejidhirisha Wilayani Chunya Mkoani Mbeya hivi karibuni baada ya Mchimbaji Mdogo wa Madini ya Dhahabu Aidan Msigwa Septemba 17, 2024 kusajili na kuuza Madini ya Dhahabu katika Soko la Madini Chunya kiasi cha kilo 111.82 zenye thamani ya shilingi bilioni 20.11
Msigwa ni mchimbaji Mdogo wa Madini ya dhahabu katika Wilaya ya Chunya anayemiliki leseni za uchimbaji mdogo (PML) na utafutaji wa madini (PL) katika maeneo tofauti Wilayani Chunya. Aidha, anamiliki mtambo wa uchenjuaji wa madini ya dhahabu wilayani humo.
Akizungumza baada ya kufanyika kwa mauzo hayo, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Chunya Mhandisi Laurent Mayalla amesema kupitia mauzo hayo, Serikali imepata kiasi cha Shilingi bilioni 1.2 ikiwa ni mrabaha, shilingi milioni 201 ada ya ukaguzi na shilingi milioni 60.34 ikiwa ni malipo ya ushuru wa huduma kwa Halmashauri na kuongeza kwamba, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepokea shilingi milioni 402.31 ikiwa ni malipo ya kodi ya zuio.
‘’Msigwa ametumia njia ya kukamatisha kwa zebaki kupata dhahabu hizo kwani mwamba huo ulionesha ni wa vikole. Ninampongeza kwa ushirikiano wake aliouonesha katika ofisi ya RMO- Chunya na taasisi nyingine katika zoezi zima la upatikanaji wa dhahabu hizo ambazo zilipelekwa sokoni kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za masoko katika kufanya biashara ya madini,’’ amesema,’’ Mhandisi Mayalla.
Ameongeza kwamba, kitendo alichokifanya Msigwa ni cha kizalendo kutokana na ushirikiano alioutoa kuanzia kwenye uchimbaji hadi uzalishaji wa dhahabu hiyo na kueleza kwamba, kinapaswa kuigwa na wachimbaji wote nchini na kwamba, suala hilo litasaidia kudhibiti utoroshaji wa madini ambayo mapato yake kwa Serikali yanasaidia kuboresha huduma nyingine muhimu.
Soko la Madini Chunya ni soko la pili kuanzishwa nchini mwezi Mei, 2019 baada ya Soko Kuu la Kwanza la Madini Geita lililoanzishwa mwezi Machi, 2019. Hadi sasa kuna jumla ya Masoko 43 ya Madini nchi nzima na Vituo vidogo vya ununuzi wa madini 105. Mkoa wa kimadini Chunya unashika nafasi ya pili kwenye uzalishaji wa dhahabu kwa wachimbaji wadogo. Katika Mwaka wa Fedha 2024/25 ofisi hiyo imepangiwa kukusanya shilingi bilioni 60.2.
Uwepo wa masoko na vituo vya ununuzi nchini umeleta nafuu kwa wauzaji na wanunuzi kukutana na kufanya biashara kwa uwazi, uwepo wa bei za elekezi, kuongezeka kwa mauzo na mapato ya Serikali, pia, yameifanya Tanzania kuwa nchi ya kuigwa kutokana na uwepo wa mfumo bora katika shughuli za uchimbaji na biashara ya madini. Taarifa za Wizara zinaonesha kuwa Mwaka wa Fedha 2023/24 kupitia masoko ya madini, kumewezesha kufanyika kwa biashara ya madini yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 2.
Kwa mujibu taarifa ya Ofisi ya Madini Chunya, shughuli za uchimbaji madini wilayani Chunya kwa asilimia kubwa zinafanywa na wachimbaji wadogo ambao wengi wanatumia zana zisizo bora pamoja na uzalishaji kwa kutumia zebaki. Aidha, wachimbaji walio wengi wanatumia teknolojia ya Vat Leaching wakati wa uchenjuaji.
Aprili 30, 2024 akisoma Hotuba ya Bajeti Bungeni, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde alisema uchumi wa madini nchini kwa kiasi kikubwa unatokana na madini ya dhahabu ambayo huchangia takribani asilimia 80 ya mapato yanayotokana na rasilimali madini.
Hakuna maoni: