ARUSHA.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watumishi wote wa Mungu, kutafakari mwenendo unaozidi kuota mizizi wa ugomvi na vurugu za aina mbalimbali miongoni mwa waumini wa imani moja wakiwemo baadhi ya viongozi wa dini.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa Kilele cha Kongamano la Nne la Uhuru wa Kidini Barani Afrika lililofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha. Amesema kwa sasa inashuhudiwa viongozi wakiondoana au kufukuzana kwenye nyumba za ibada kwa sababu mbalimbali zikiwemo matumizi mabaya ya fedha na mali za kanisa, kugombea madaraka, kuajiriana kwa upendeleo, rushwa na kukosekana kwa haki kwenye chaguzi.
Amesema Viongozi wa dini wanayo nafasi na heshima ya pekee katika jamii hapa Tanzania na nchi nyingine za Afrika, kama wawakilishi wa Mungu hapa duniani hivyo ni jambo la muhimu kudhibiti tamaa ya mali iliyopitiliza na uchu wa madaraka na kurudi kwenye wito halisi. Ametoa rai na kuwasisitiza kurudi kwenye utaratibu wa kusemana na kuonyana kwa upendo kanisani na misikitini badala ya kufanya hivyo mitandaoni.
Makamu wa Rais ametoa wito wa kutafakari hali ya ya baadhi ya viongozi wa dini au dhehebu moja kujiambatanisha na chama kimojawapo cha siasa na kupelekea maoni yao binafsi ya kisiasa kutafsiriwa kuwa ndiyo maoni ya dini au dhehebu wanaloliongoza. Amesema hali hiyo inapelekea changamoto kubwa katika uhusiano na mashirikiano baina ya Serikali ambayo haina dini na baadhi ya viongozi wa dini wenye mrengo dhahiri wa kisiasa.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi Viongozi wa dini kuhimiza umuhimu wa kuishi katika hali ya usalama na amani na mazingira kama njia mojawapo ya kudumisha uhuru kwa kidini kwa kuwa mazingira na rasilimali zake kama vile maji ni muhimu katika kumwabudu Mungu na kuwezesha binadamu, wanyama, mimea, ndege na wadudu kuishi pamoja kwa amani na kwa kutegemeana.
Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa viongozi wa dini na washiriki wote wa Kongamano hilo, kusimamia kikamilifu suala la maadili mema katika jamii, kwa kuanzia kwa wazazi/walezi hadi kwa vijana na watoto. Amesisitiza suala la kuhakikisha wanakuwepo walimu wa dini katika muda unaotolewa mashuleni ili kutunza na kurithisha maadili mema kwa vizazi vya sasa na vijavyo na kukemea maovu kwa nguvu zote.
Makamu wa Rais amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye amani na utulivu katika Bara la Afrika ambapo Kiini cha hali hiyo ni misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa iliyosisitiza umoja, mshikamano, kuheshimiana na kuondoa tofauti za kidini, kisiasa, rangi au kabila. Sambamba na hilo amesema uhuru wa kidini hapa nchini unatambuliwa na kulindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali inashirikiana kwa karibu na viongozi wa dini zote nchini hasa katika sekta za afya na elimu na kushauriana kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza na kuhakikisha shughuli za dini zinaendeshwa kwa amani na utulivu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato, Unioni ya Kaskazini mwa Tanzania Mch. Mark Malekana amesema malengo ya kongamano hilo ni kuhimiza amani, heshima ya binadamu, haki za binadamu na uhuru wa dhamira miongoni mwa Waafrika. Amesema pamoja na tofauti zilizopo za itikadi, imani, utamaduni na rangi ni muhimu kutambua jambo muhimu la kutuunganisha ni sisi sote ni binadamu.
Amesema Kongamano hilo limedhamiria kuhimiza Afrika inayopendana, na inayoheshimiana.
Kongamano la Nne la Uhuru wa Kidini la Afrika lilianza tarehe 17 Septemba 2024 limehusisha mataifa yote ya Bara la Afrika na kuhudhuriwa na Wanasheria, Majaji, Wanadiplomasia, Viongozi waandamizi mbalimbali, Wasomi kutoka Taasisi mbalimbali za Afrika, wawakilishi wa Mahakama, wawakilishi wa Umoja wa Afrika pamoja na Viongozi wa dini mbalimbali.
Hakuna maoni: