NBS, OCGS ZATAKIWA KUZINGATIA MUDA WA TATHMINI YA PSSN II.

 




Na Mwandishi Wetu, 

Zanzibar. 

OFISI ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar (OCGS) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS), zimetakiwa kukamilisha kwa wakati zoezi laTathmini ya Mwisho ya Kupima Matokeo ya Kipindi cha Pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN II) ya Mwaka 2024/2025.

 Aidha mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar inatarajiwa kuhusika na utafiti huo ambao utaonesha maeneo yote ambayo yameguswa na PSSN II.

Kauli yakuzitaka OCGS na NBS kukamilisha tathmini ya PSSN II inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Hemed Suleimani Abdulla wakati akizundua tathmini ya mwisho ya mpango huo katika Ukumbi wa Idris Abdul Wakil, Kikwajuni.

Makamu wa Rais Abdulla amesema iwapo taasisi hizo muhimu kwa utafiti nchini zitatekeleza jukumu hilo kwa weledi ni wazi ripoti ya thathmini itakuweza kusaidia Serikali na wadau mbalimbali kutumia kwenye mipango ya maendeleo endelevu.

“Zoezi la kufanya tafiti linakuwa si rahisi lakini kutokana na umahiri wenu mmeweza kufanya kazi hii ya maandalizi na kuikamilisha kwa wakati kama ilivyopangwa. Aidha, napenda kuzipongeza Benki ya Dunia (WB) na TASAF kwa ushirikiano wao mkubwa wa kiufundi na kutoa miongozo mbalimbali wakati wote wa maandalizi ya shughuli hii,” amesema.

Amesema madhumuni ya tathmini hii ni kuweza kupima endapo mpango huu unafikia malengo yaliyokusudiwa ya kuondoa umaskini kwa kaya zilizoainishwa kuishi katika umaskini uliokithiri.

“Tathmini kama hizi hufanyika katika nchi mbalimbali zinazotekeleza mipango kama hii duniani kupitia taasisi za fedha na maendeleo za kimataifa.

Katika nchi yetu, mpango huu unahusisha mikakati zaidi ya mmoja katika utekelezaji ili kuhakikisha kwamba walengwa wanafaidika na kutoka katika hali ya umasikini mapema zaidi.

Abdulla amesema matarajio yake ni kwamba, tathmini hiyo itaweza kutoa taswira halisi ya hali ilivyo na kuiwezesha Serikali kuona ni eneo lipi tunafanya vizuri zaidi na eneo lipi linahitaji kuongeza mkazo,” amesema.

Amesema kama ulivyokuwa kwa tathmini ya awali, Serikali inapenda kuona tathmini ya mwisho inawapatia takwimu zenye ubora zitakazowaonesha mwenendo wa viashiria mbalimbali vya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini nchini.

Akifafanua kuhusu tathmini hiyo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Salum Kassim Ali amesema tathmini hiyo inafanyika baada ya ile ya awali ambayo ilifanyika mwaka 2022 na hii awamu ya mwisho inafanyika huu mwaka wa 2024.

“Katika tathmini hii jumla ya mikoa 17 itahusika ambapo mikoa 14 Tanzania Bara na mikoa mitatu Zanzibar yenye jumla ya shehia, vijiji na mitaa 434. Kati ya hiyo, vijiji na mitaa 376 ni kutoka Tanzania Bara na shehia 58 ni kutoka Zanzibar,” amesema.

Ali ametaja mikoa itakayofanyiwa utafiti ni Kaskazini Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kusini Pemba upande wa Zanzibar na Mtwara, Lindi, Dodoma, Ruvuma, Iringa, Pwani, Singida, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Katavi, Rukwa na Dar Es Salaam Tanzania Bara.

Amesema Mpango wa Kunusuru kaya Maskini umefanyika kwa awamu mbili ambayo Awamu ya Kwanza (PSSN I) uliotekelezwa kuanzia Mwaka 2012 hadi Mwaka 2019, ukilenga kufikia takribani kaya milioni 1.2 yaani asilimia 15 ya kaya zote za Tanzania kwa wakati huo.

Ali alisema mpango huo ulihusisha kaya zote zinazoishi chini ya mstari wa umaskini wa chakula na wale walio katika hatari ya kuangukia chini mstari wa umaskini wa chakula.

Hivyo, Awamu ya Kwanza iliweza kufikia lengo lake la kuwafikia wananchi waliokusudiwa katika asilimia 70 ya shehia, vijiji na mitaa yote hapa nchini. 

“Kwa sasa, Serikali ya Tanzania inatekeleza PSSN II iliyokuwa na lengo kuzifikia kaya milioni 1.4 katika shehia, vijiji na mitaa yote hapa nchini jambo ambalo limefanikiwa,” amesema.

Amesema mpango unatoa ruzuku ya msingi kwa kaya za walengwa ambazo pia zinapaswa kutimiza masharti ya elimu na afya, pia, kaya hizo zinanufaika kwa kushiriki katika miradi ya jamii yenye lengo la kutoa fursa za ajira za muda.

“Katika utekelezaji wa Mpango wa Kuweka Akiba na Kuwekeza, kaya za walengwa wanapata mafunzo ya stadi za ujasiriamali na mbinu za kuunda vikundi endelevu vya kuweka akiba na kuwekeza. 

Vile vile, miradi ya kuendeleza miundombinu ya afya, elimu, barabara, kilimo, mazingira na maji inatekelezwa na walengwa kupitia mpango huu,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray amesema PSSN II ilizinduliwa Mwezi Februari 2020, ukiendelea kuhudumia takribani kaya milioni I.4 zenye zaidi ya kaya milioni 6 na utekelezaji wake unafanyika katika vijiji, mitaa na shehia zote nchini.

“Madhumuni ya PSSN II ni kuwezesha kaya za walengwa kutumia fursa za kuongeza kipato, huduma za jamii na kuwekeza katika kuendeleza rasilimali watu hususan watoto,” amesema.

Mziray amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2024, Mpango umehawilisha ruzuku ya zaidi ya Sh. bilioni 945.5 kwa kaya za walengwa.

Amesema TASAF inatekeleza Mpango wa Kutoa Ajira za Muda (PWP) kwa kaya za walengwa, ambapo kwa kipindi hiki jumla ya miradi 27,863 iliibuliwa na wananchi na kutekelezwa na walengwa wa mpango na kiasi cha Sh.bilioni 117.3 zimetumika kulipa ujira kwa kaya za walengwa 662,374 kwa kushiriki katika kutekeleza miradi.

Mkurugenzi huyo amesema miradi hiyo ilikuwa inahusu kutengeneza miundombinu yenye faida kwa jamii nzima kama miradi ya umwagiliaji, upandaji miti, mabwawa, utunzaji wa ardhi, na barabara zinazounganisha vijiji, mitaa au shehia na barabara kuu.

Mziray amesema pia katika kukuza uchumi wa kaya hadi Juni 2024 kulikuwa na jumla ya vikundi 60,342 vyenye wanachama 838,241, kati ya wanachama hao, wanawake ni 716,515 sawa na asilimia 84.5 na wanaume ni 121,726 asilimia 14.5.

Amesema vikundi hivyo vimekusanya akiba ya Sh bilioni 7.9 na kukopeshana Sh bilioni 3.2 kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza miradi inayowaongezea kipato, huku kaya 84,674 zikipewa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara na kupatiwa ruzuku ya kuanzisha shughuli za kiuchumi yenye thamani ya Sh bilioni 31.3 hadi kufikia Juni 2024.9.21

Naye Msimamizi wa Mradi na Mwakilishi wa WB, Claudia Zambra amesema mpango huo wa PSSN II umekuwa na mafanikio makubwa jambo ambalo linawapa nguvu ya wao kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia TASAF kuwainua Watanzania.

“Mpango unaenda kwenye tathmini lakini kwa namna tunavyoona kupitia walengwa tunaona umefanya vizuri, naamini watafiti watakuja na matokeo mazuri na kuonesha nini cha kuboresha,” amesema.




Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.