NLD YATANGAZA OPERESHENI YA "FYEKA CCM" NA KUTAMBULISHA WANACHAMA WAPYA.



DAR ES SALAAM.

Chama Cha National League For Democracy (NLD) kimeanzisha operesheni mpya inayoitwa "Fyeka Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2024/2025," katika hafla ya utambulisho wa wanachama wapya iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe Septemba 29 2024. Miongoni mwa wanachama wapya ni Mariam Sijaona, aliyekuwa Naibu Katibu Mwenezi Ngome ya Wanawake na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Kanda ya Pwani kutoka ACT Wazalendo.


Katika hafla hiyo, pia alitambulishwa Scola Kahana, aliyekuwa mgombea ubunge wa Kibaha Mjini kupitia chama cha Alliance for Democratic Change (ADC). Doyo, kiongozi wa NLD, alisisitiza umuhimu wa kufanya siasa safi na kuheshimu viongozi, akionya dhidi ya lugha chafu na dhihaka katika siasa.


"Hatuna budi kuendeleza siasa za heshima na amani. Mambo ya kutukana yamekuwa yakikithiri, na hatuwezi kukubali hali hii katika siasa zetu," alisema Doyo.


Aidha, aliomba Ofisi ya Rais Tawaka za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuongeza muda wa kampeni, akisema wiki moja ni fupi kwa vyama vya siasa kujipanga. 


Doyo alieleza kwamba operesheni hiyo itafanyika katika mikoa kumi, ikiwemo Tanga, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Singida, Dodoma, Mwanza, na Kagera, huku wakijipanga kuandaa wagombea kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.


Mariam Sijaona alithibitisha kujiunga na NLD bila kushawishiwa, akieleza kwamba amefanya kazi kubwa katika kuimarisha ACT, na anatarajia kushirikiana na NLD katika uchaguzi ujao. 


Hii ni hatua muhimu kwa NLD katika harakati zake za kutafuta nafasi ya kisiasa nchini, ikionyesha dhamira yake ya kukabiliana na CCM kwa kuzingatia sera na itikadi zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.