Na Mwandishi wetu,
Dar es salaam.
Tanzania inakaribia kuadhimisha Siku ya Mbolea Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 13 ambapo Mamlaka ya Kudhibiti Mbolea nchini (TFRA) imesema inatekeleza juhudi mbalimbali kuboresha uzalishaji wa kilimo Tanzania kupitia ruzuku ya mbolea, hatua ambayo imehamasisha wakulima wengi kuongeza matumizi ya mbolea na hivyo kuongeza tija.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 1/ 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Jeol Lawrent alieleza kuwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika kwa namna ya kipekee katika Mkoa wa Manyara, na yatatanguliwa na Kongamano Kuu Jijini Dodoma.
Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Mbolea litafanyika tarehe 11 na 12 Oktoba 2024, katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma, likitarajia kuwakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi ili kujadili changamoto zinazokabili tasnia ya mbolea na wakulima. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, atakuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo.
Mada zitakazojadiliwa zitahusisha usimamizi bora wa mbolea, tathmini ya mifumo ya udhibiti, na mchango wa afya ya udongo katika usalama wa chakula nchini. Aidha, kongamano litakazia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika kusimamia tasnia ya mbolea, kuhamasisha uzalishaji wa ndani, na biashara ya mbolea katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC.
Waziri wa Kilimo, Mh. Hussein Bashe, atazindua Mkakati wa Maendeleo ya Tasnia ya Mbolea nchini Tanzania jioni ya Oktoba 11.
Wakati kongamano likiendelea Dodoma, maadhimisho mkoani Manyara yatafanyika kuanzia Oktoba 10-12, yakihusisha maonyesho kutoka wadau wa sekta ya kilimo, hasa katika mnyororo wa thamani wa mbolea. Maonyesho haya yatafanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Babati, yakihusisha washiriki zaidi ya 45 wakionesha bidhaa za kilimo na kutoa mafunzo kupitia shamba darasa.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mh. Queen Sendiga, atakuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maonyesho, huku Waziri wa Kilimo Mh. Hussein Bashe akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika siku ya kilele.
Kwa mujibu wa Bw. Louis Kasera, Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku Taifa na Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani, amesema matumizi ya mbolea nchini yameongezeka hadi tani 840,000 kwa mwaka, ukilinganisha na tani 360,000 mwaka wa 2021/2022, kipindi ambacho mpango wa ruzuku ya mbolea ulianza.
Kasera alisisitiza kwamba ongezeko hilo limetokana na wakulima kuhamasika kutumia ruzuku ipasavyo. TFRA pia imefanikiwa kudhibiti mbolea feki kupitia mfumo wa kidijitali, ambao unasaidia kufuatilia mchakato mzima wa usambazaji na kuwatambua wasambazaji wa mbolea zisizo na ubora na kuwafwatilia hatua kwa hatua.
Hakuna maoni: