RC CHALAMILA AZINDUA KONGAMANO LA NISHATI SAFI DAR ES SALAAM.



DAR ES SALAAM.

Leo, Septemba 12, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, ameanzisha kongamano la matumizi ya nishati safi ya kupikia katika viwanja vya Karimjee, Jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Wilaya, Mameya, Wakurugenzi wa Halmashauri, watendaji wakuu wa taasisi za nishati safi, viongozi wa dini, pamoja na mamia ya mama lishe na baba lishe.


Katika uzinduzi wa kongamano hilo, RC Chalamila alitumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa kampuni ya Lake Gas kwa kutoa mitungi 1000 ya gesi kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kupunguza matumizi ya nishati chafu na kuhamasisha matumizi ya nishati safi. Alisisitiza umuhimu wa taasisi na mashirika mengine kuiga mfano wa kampuni ya Lake Gas kwa kutoa mitungi zaidi ya gesi ili kufikia wananchi wengi zaidi.


Kwa kuongeza, RC Chalamila alitangaza Tamasha la Mapishi kwa kutumia nishati safi litakalofanyika Septemba 23, 2024. Tamasha hili litaonyesha mapishi mbalimbali kama nyama choma, mbuzi choma, samaki choma, na pilau. Aidha, aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi na aliahidi kutoa ofa maalum kwa watu 1000 wa kwanza kufika kwenye tamasha hilo. Eneo la tamasha litajulishwa siku za usoni.


RC Chalamila pia aliagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuratibu upatikanaji wa mitungi ya gesi kutoka taasisi za serikali, na lengo ni kuchangia mitungi 200 hadi 300 kabla ya Septemba 30, 2024.


Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Lake Gas, Bw. Stephen Mtemi, alisisitiza kuwa kampuni yao itaendelea kushirikiana na mkoa wa Dar es Salaam na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan. Aliwashukuru Wizara ya Nishati na Wakala wa Nishati Vijijini kwa kusaidia usambazaji wa majiko ya gesi na kuhamasisha Watanzania kutumia nishati safi.





Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.