SERIKALI YAHAIDI KUIMARISHA MIFUMO YA AFYA KWA KUTAMBUA HUDUMA ZA UTENGAMAO: KONGAMANO LA PILI LA HUDUMA ZA UTENGAMAO KUFANYIKA DAR ES SALAAM.


Na Mwandishi Wetu,

Dar es salaam.

Wizara ya Afya nchini inazidi kuimarisha mfumo wa afya nchini kwa kuzingatia umuhimu wa huduma za utengamao. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Tiba, Dkt. Hamad Nyembea, wakati wa mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa kwa ajili ya maandalizi ya Kongamano la Pili la Huduma za Utengamao la Afya.


Kongamano hili, litakalofanyika kuanzia Septemba 18 hadi 20, 2024, katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam, lina kaulimbiu ya "Kuendeleza Ajenda ya Utengamao wa Afya Nchini Tanzania: Kuimarisha Mifumo ya Afya." 


Dkt. Nyembea alisisitiza kuwa huduma za utengamao ni muhimu katika kusaidia wagonjwa walio na majeraha au magonjwa ya muda mrefu, kwa kutoa matibabu ya muda mrefu, msaada wa kisaikolojia, na huduma za urekebishaji wa viungo. Huduma hizi ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuboresha huduma za afya kwa Watanzania wote, bila kujali hali zao au maeneo wanakoishi.


Aidha, Dkt. Nyembea alisisitiza kuwa huduma za utengamao siyo hiari bali ni hitaji muhimu katika kuhakikisha mfumo wa afya una uwezo wa kuwasaidia wananchi kwa kina. Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Rehab Health, MDH, Jeshi la Polisi, na sekta binafsi kama Benki ya CRDB, ili huduma hizi zipanuke na kuwafikia wananchi wengi zaidi, hasa wale walioko vijijini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Rehab Health, Remla Shirima, alitangaza kuwa kongamano hilo litawakutanisha wataalam, watunga sera, na watoa huduma za afya kwa ajili ya kujadili na kuvumbua mikakati bora ya huduma za utengamao wa akili. Aliwataka wadau wa afya na maendeleo kushiriki katika kongamano hilo ili kuleta mabadiliko chanya katika huduma za afya.

Kwa taarifa zaidi, kongamano hili litahudhuriwa na Mheshimiwa Waziri wa Afya kama mgeni rasmi, ikiwa ni ishara ya dhamira ya wizara katika kuboresha mfumo wa afya.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.