SHIRIKA LA JHFMRI LAPONGEZWA KUWEZESHA WASICHANA ZAIDI YA LAKI 2 MBEYA

Maafisa Maendeleo waagizwa kuhakikisha vikundi vya wasichana hao vinasajiliwa ili wapate mikopo ya Halmashauri.

Na WMJJWM, 

Mbeya.

Serikali imelipongeza Shirika la JHFMRI kwa kuwasaidia wasichana wanaoishi mazingira hatarishi kubadilika tabia na kuwezeshwa kiuchumi, kielimu na kisaikolojia kupitia mradi wa Dreams.



Hayo yamebainika wakati wa mdahalo wa pamoja wa BINTI JASIRI kwa wasichana wanaonufaika na mradi huo jijini Mbeya Septemba 11, 2024.



Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera akifungua mdahalo huo, amewahakikishia wasichana walioshiriki kwamba Serikali ya Mkoa wa Mbeya itawapa kipaumbele katika utoaji wa mikopo ya mapato ya ndani ya Halmashauri itakayowainua zaidi kiuchumi na kufikia ndoto zao za kusaidia familia na Taifa.


Mhe. Homera amewaelekeza maafisa Maendeleo ya Jamii mkoani humo kuhakikisha wasichana hao wanaunda vikundi na kusajiliwa na amewataka wasichana kuanza taratibu za kupata vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya Taifa ili viwasaidie kutambulika na taasisi mbalimbali zenye fursa.


Akizungumza katika ufunguzi wa Mdahalo huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amelipongeza Shirika hilo na kusema mabinti hao wakiwezeshwa watatoa mchango mkubwa kwa familia na taifa. 


"Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ikiwemo wasichana, ni ajenda kubwa ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, hivyo wadau mnatekeleza ajenda hiyo. Kwa wafanyabiashara ndogondogo, Rais Samia ametoa sh. Bil. 18 hivyo mjisajili kupata fursa hiyo" amesema Mpanju.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Toufiq pamoja na mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Michael Kimbaki, wametambua juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mabinti wanawezeshwa kwa faida ya kwani wakijengewa uwezo wa kiuchumi itasaidia kupambana na ukatili dhidi ya watoto na wanawake kwani ndio waathiriwa wakubwa hasa miaka 15-25.



"Kazi inayofanywa na Shirika hili ya kuwajengea uwezo wasichana hawa ni kazi ya kujenga taifa lijalo, watu shujaa na jasiri kuweza kulikomboa Taifa. amesema Mhe. Fatma



Dorcas Binala mmoja wa wanufaika wa mradi wa Dreams amesema wasichana zaidi ya laki 2 wamefikiwa tangu mradi huo uanze mwaka 2016 ambapo wakisajiliwa huaptiwa huduma mbalimbali za msingi na ziada ikiwemo elimu ya kupambana na maambukizi ya VVU, mabadiliko ya tabia, matumizi ya fedha, Uzazi wa mpango, matibabu, elimu ya malezi na makuzi na kuimarisha uchumi ili kujitegemea wenyewe.





Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.