TPA YASHINDA TUZO YA BANDARI BORA AFRIKA MASHARIKI

 





Na Mwandishi Wetu,

Mwanza.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA imetunukiwa tuzo ya ushindi wa jumla katika maonesho ya 19 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya furahisha Mkoani mwanza na kushirikisha zaidi ya taasisi nyingine 200 kutoka nchi wanachama.

Vilevile TPA imekuwa mshindi wa kwanza kati ya Taasisi za Serikali zilizoshiriki kwenye maonesho hayo kwa kuwa na banda bora lenye kuvutia zaidi katika maonesho hayo.

Akiongea wakati wa kutoa tuzo kwa TPA wakati wa maonesho hayo , Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Selemani Jafo amesema tuzo hiyo ya TPA imetokana na uboreshaji wa huduma katika bandari inazozisimamia kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika.

“Mafanikio haya ni matokeo ya usimamizi mzuri unaofanywa na TPA ikiwemo ukiwemo uwekezaji unaofanyika katika banadri ya Dar es Salaam,” amesema Waziri Jafo katika maonesho hayo yenye kauli mbiu ya "Uboreshaji wa Mazingira ya uwekezaji na Baishara ni Kichocheo katika kukuza Uchumi wa Nchi".

Maonesho hayo yana lengo la kukuza fursa za biashara na kuziwezesha nchi wanachama wa Afrika Mashariki kuchangamkia fursa ya masoko ya jumuiya nyingine ikiwemo vile SADC.

Akiongea wakati wa kufunga maonesho hayo, Waziri Jafo amesema malengo ya Serikali ni kuboresha upatikanaji wa huduma katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara, reli na anga ili kukuza ukuaji wa biashara na uchumi.

Pia amesema kuwa uwekezaji mkubwa umefanyika katika bandari ya Dar es Salaam, Mwanza na maeneo mengine ili kurahisisha wafanyabiashara wa ndani nan je ya nchi kusafirisha biashara zao kwa haraka na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akiongelea mfano wa bandari ya Dar es Salaam, amesema uwekezaji uliofanyika katika bandari hiyo ambayo ni kiungo kikubwa kwa zaidi ya nchi nane zisizo na pwani katika Afrika Mashariki, Kusini, na Kati umepelekea kuongezeka ufanisi mkubwa katika kuhudumia shehena za meli za mizigo zinazotia nanga bandarini hapo.

Bandari ya Dar es Salaam pia ni kiungo muhimu cha usafirishaji wa mizigo kwenda Mashariki ya Kati, Ulaya na hata bara la Amerika.

“Uwekezaji huu mkubwa umepelekea upatikanaji wa huduma bora na ufanisi wa hali ya juu”,

“Na hii imevutia wateja zaidi kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa inayofanyika katika bandari zetu,” alisema Waziri Jafo.

Aliongeza kuwa maboresho makubwa katika miundombinu ya bandari yameimarisha ubora wa huduma zinazotolewa ikiwemo kushusha na kupakia mizigo.

 “Uwekezaji huu umepunguza muda wa kuhudumia meli kutoka siku 7 hadi kati ya siku 3 na 4, kutokana na uboreshaji wa huduma uliofanyika,” alisema Waziri.

Alisema uwekezaji huu pia umepunguza kwa kiasi kikubwa muda wa meli kusubiri kuingia bandarini kutoka siku 5 hadi siku 3.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TPA, Bw. Leonard Magomba, alisema kuwa TPA sasa ina malengo zaidi ya kuboresha bandari zake nyingine kupitia upanuzi wa miundombinu, uwekezaji katika vifaa, na kuajiri wataalamu ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya kimataifa vya utoaji huduma.

“Kwa sababu ya uwekezaji huu mkubwa, Bandari ya Dar es Salaam sasa inaweza hata kupokea meli kubwa zenye urefu wa hadi mita 300,” alisema Magomba.

“Hii imewezekana kwa kupanua kina cha lango la kuingia bandarini na eneo la kugeuzia meli, hali inayowezesha meli kubwa kutia nanga kwa urahisi zaidi.”

Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wateja, wadau, na umma kutembelea banda la TPA katika maonyesho hayo ili kuongeza ufahamu wao kuhusu huduma zinazotolewa na bandari hizo.

Magomba pia alihimiza wafanyabiashara kuendelea kutumia bandari za hapa nchini kwa mahitaji yao ya usafirishaji wa mizigo ili kunufaika na fursa zilizopo na ufanisi ulioboreshwa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.