S!TE 2024: KITOVU CHA UTALII KIMATAIFA KUFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM KUANZIA OKTOBA 11.


Na Mwandishi wetu,

Dar es Salaam.

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) inatarajiwa kufanya onyesho la nane la Swahili International Tourism Expo (S!TE) kuanzia Oktoba 11 hadi 13, 2024,Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Taarifa hii imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Ephraim Mafuru, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.


S!TE 2024 ni jukwaa muhimu kwa watoa huduma wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi, ambao watapata fursa ya kuonesha bidhaa zao na kujenga mitandao ya biashara. Onesho hili linaendana na sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 na mkakati wa kutangaza utalii kimataifa wa mwaka 2020-2025, unaolenga kutangaza Tanzania kama kivutio bora cha utalii duniani.


Aidha, Mafuru amesisitiza kuwa S!TE ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano III (FYDP III 2021/22-2025/26), ambapo utalii wa mikutano na matukio (MICE Tourism) umeainishwa kama kipaumbele cha kimkakati. Lengo ni kuvutia watalii milioni tano na kupata mapato ya Dola za Marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.


"Onesho la mwaka huu litakuwa na waoneshaji zaidi ya 120 wa bidhaa na huduma za utalii pamoja na wanunuzi wa kimataifa 120 kutoka masoko muhimu ya utalii kama Ulaya, Asia, na Amerika. Pamoja na hayo, ziara za mafunzo (FAM trips) zitafanyika kufungua kanda za utalii zinazochipukia, ikiwa ni pamoja na Ukanda wa Magharibi na Kusini wa Tanzania, na kuunganisha shughuli za utalii za Zanzibar na Tanzania Bara.


Mafuru aliwaomba Watanzania na vyombo vya habari kushiriki katika kuhamasisha na kutangaza S!TE 2024, ili kuwafikia wadau wengi zaidi na kunufaika na fursa zitakazojitokeza katika onesho hili.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.