ZAIDI YA ASILIMIA 99.75 YA VYETI VIMEHAKIKIWA.


Na wandishi wetu, 

Dar es Salaam.


Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Frank Kanyusi, amewataka wananchi na waombaji wote wa mikopo ya elimu ya juu kutosubiri dirisha la mikopo kufunguliwa ili waanze kutuma maombi ya uhakiki RITA. Badala yake, wanashauriwa kutuma maombi mapema kwani mfumo wa kuhakiki vyeti upo wazi mwaka mzima.


Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hafla ya kubadilishana hati za makubaliano iliyojumuisha taasisi zinazohusika na masuala ya utambuzi, ambazo ni Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), na CREDITINFO Tanzania Ltd, ambayo ni taasisi ya uchakataji wa taarifa za waombaji mikopo katika taasisi za fedha, Kanyusi alisema:


“Kwa sasa, mwombaji mkopo anatuma maombi ya uhakiki wa cheti cha kuzaliwa au cha kifo cha mzazi wake kupitia mfumo wa TEHAMA wa eRITA unaopatikana kupitia tovuti ya wakala ya www.rita.go.tz. Baada ya uhakiki kukamilika, tunampatia mwombaji NAMBA MAALUM ambayo akiingiza kwenye mfumo wa Bodi ya Mikopo – inasomeka RITA moja kwa moja,” alisema Kanyusi.


Kanyusi alibainisha kuwa tangu dirisha lilipofunguliwa tarehe 1 Juni 2024, wamepokea jumla ya maombi ya uhakiki 244,354, ambapo kati ya hayo, maombi 218,263 ni ya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na 26,091 ya uhakiki wa vyeti vya vifo.


“Hadi kufikia leo, Wakala umeshahakiki jumla ya maombi 243,629 sawa na asilimia 99.75 ya maombi yaliyopokelewa. Kati ya maombi yaliyofanyiwa uhakiki, jumla ya maombi 26,150 yalikuwa na mapungufu na waombaji walirudishiwa kwa ajili ya kufanya marekebisho, na maombi 618 yalikataliwa kwani vyeti vilivyowasilishwa kwa ajili ya uhakiki havikuwa halali,” alisema Kanyusi.


Aidha, Kanyusi alisema maombi 725 bado yanaendelea kuhakikiwa na zoezi linategemewa kukamilika ndani ya siku moja.


“Katika kuhakikisha azma ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi inatimia sambamba na kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutaka mifumo ya yote ndani ya serikali kusomana ifikapo Desemba mwaka huu, RITA kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB) tumeshalitekeleza agizo hilo,” alisema Kanyusi.


Aliongeza kuwa wakala wamejipanga kutekeleza yote yaliyomo kwenye makubaliano na HESLB sambamba na kufanya maboresho ya mfumo wa uhakiki, lengo ikiwa ni kuongeza ufanisi katika utendaji.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.