Veronica Simba, WMA Dodoma.
Imeelezwa kuwa ujenzi unaoendelea wa Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo (WMA) unatarajiwa kukamilika Januari 2025.
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa WMA, Karim Zuberi amemweleza hayo Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya aliyefanya ziara kujionea maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo eneo la Medeli jijini Dodoma, Septemba 27, 2024.
Akiwasilisha taarifa fupi kwa Katibu Tawala, Zuberi amesema Mkandarasi amebakiwa na wiki 14 kukamilisha Mradi huo wa miaka miwili na nusu wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni sita za kitanzania (TZS 6.17)
“Kutokana na kazi iliyofanyika hadi sasa, Mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 3.8 sawa na asilimia 61.6 ambapo Mradi umefikia asilimia 79.4”
Aidha, Zuberi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuidhinisha bajeti ya mapato ya ndani katika kutekeleza Mradi huo.
Ametaja miongoni mwa manufaa yatakayopatikana baada ya jengo hilo kukamilika kuwa ni pamoja na kuongeza morali ya kazi kwa wafanyakazi wa WMA kutokana na uwepo wa mazingira mazuri ya Ofisi.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mmuya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya WMA Mkoa wa Dodoma, pamoja na kupongeza kazi nzuri inayoendelea kufanyika, amemsisitiza Mkandarasi pamoja na Mshauri Elekezi kuzingatia viwango vya ujenzi wa majengo ya Serikali.
Akifafanua, Mmuya amesema pamoja na mambo mengine, ni muhimu kuhakikisha miundombinu mbalimbali ya jengo hilo inakuwa wezeshi kwa watu wenye ulemavu.
Tangu kuanza kwa ujenzi wa Jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo Julai 2, 2022, viongozi mbalimbali wametembelea kukagua maendeleo yake akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ambaye aliweka Jiwe la Msingi Februari 6, 2024.
Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo aliyetembelea na kukagua Mradi Julai 17, 2024, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji (Agosti 24, 2023) pamoja na Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dkt. Hashil Abdallah (Januari 3, 2023)
Mradi wa Ujenzi wa Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo unasimamiwa na Mshauri Elekezi MUST Consultancy Bureau Limited na kutekelezwa na Mkandarasi kampuni ya Mohammedi Builders Limited.
Ofisi za WMA zipo katika mikoa yote Tanzania Bara ambapo jukumu lake kuu ni kuzilinda pande mbili yaani mlaji na muuzaji wa bidhaa na huduma kupitia matumizi sahihi ya vipimo.
Hakuna maoni: