MIRADI YA MIUNDOMBINU WILAYANI ILEJE KUKAMILIKA KWA WAKATI – KASEKENYA.

 






Naibu Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Ileje, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewahakikishia wazee wa Wilaya ya Ileje kuwa miradi ya miundombinu ya barabara, maji, umeme, shule, zahanati, na vituo vya afya inayoendelea kujengwa jimboni humo itakamilika kwa wakati.

Akizungumza na wazee hao kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya miradi ya miundombinu inayoendelea wilayani Ileje, mkoani Songwe, Mhandisi Kasekenya alisema kuwa Serikali imedhamiria kufungua wilaya ya Ileje katika nyanja zote za miundombinu ili kuchochea maendeleo na kukuza uchumi wa wilaya hiyo kongwe.

“Wazee wangu, Serikali imejipanga kuhakikisha miradi ya miundombinu inajengwa na kumalizika kwa wakati, hivyo ni muhimu wahamasisheni vijana kuchangamkia fursa za ajira na uwekezaji katika miradi hii,” alisema Mhandisi Kasekenya.

Aidha, Naibu Waziri huyo alizungumzia umuhimu wa wazee wa wilaya hiyo kutoa elimu kwa vijana kuhusu umuhimu wa kupanda miti na kuitunza ili kulinda uoto wa asili. Alisisitiza kuwa kilimo cha miti, pamoja na biashara ya miti na mbao, itakuwa ni fursa kubwa ya kukuza uchumi wa Ileje na Taifa kwa ujumla.

Kasekenya aliongeza kuwa Wilaya ya Ileje itaendelea kufunguliwa kwa miundombinu bora ya barabara ambazo zitakamilika na kupitika wakati wote, hivyo kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji wilayani humo.

Kwa upande wake, Mchungaji Msokwa Saston, akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake, alimshukuru na kumpongeza Mbunge wa Ileje kwa namna anavyothamini wazee na kuwashirikisha katika mipango ya maendeleo na utunzaji wa mazingira. Alimuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha matarajio ya wananchi wa Ileje yanafikiwa.

Ziara ya kukagua miundombinu wilayani Ileje ni sehemu ya mkakati wa Mbunge huyo kushirikisha makundi mbalimbali ya kijamii kuona na kuthamini kazi zinazofanywa na Serikali katika wilaya hiyo.





..

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.