MWENYEKITI MPYA WA TUME YA MADINI AWATAKA MAAFISA MADINI WAKAZI WA MIKOA KUONGEZA USIMAMIZI WA MAZINGIRA KWENYE SHUGHULI ZA MADINI.
Mwenyekiti mpya wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuongeza usimamizi wa mazingira kwenye shughuli za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea na kusababisha vifo kwa wananchi.
Lekashingo ametoa rai hiyo mapema leo Novemba 18, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye kikao chake na menejimenti ya Tume ya Madini ikihusisha Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo, Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa chenye lengo la kuweka mikakati ya kuimarisha Sekta ya Madini hasa kwenye eneo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka 2024/2025.
Sambamba na kupongeza kwa kasi ya ukusanyaji wa maduhuli inayofanywa na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ameongeza kuwa ni vyema suala la usimamizi wa mazingira kwenye shughuli za madini likazingatiwa ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini zinafanyika pasipo kuathiri mazingira.
Aidha, amewataka maafisa hao kuendelea kutatua changamoto nyingine katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na migogoro kati ya wachimbaji wa madini na jamii inayowazunguka, kiteknolojia na kuongeza ubunifu kwenye utendaji kazi.
Pia amewataka kuendelea kushirikiana kama timu moja na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto zilizopo katika Sekta ya Madini.
Naye Mwenyekiti wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ambaye ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, Mayigi Makolobela akizungumza kwa niaba ya maafisa hao, amepongeza uteuzi wa mwenyekiti mpya na kuongeza kuwa siri ya uteuzi wake ni kutokana na historia nzuri ya utendaji kwenye Sekta ya Madini.
Hakuna maoni: