
Na Mwandishi Wetu,
Dar es salaam.
Chuo cha Ufundi Stadi cha Furahika, kilichopo jijini Dar es Salaam, kimeanzisha kozi mpya ya kuwafundisha wasichana kutoa huduma kwenye mabasi na daladala kama ukondakta.
Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. David Msuya, ameibainisha hayo tarehe 5 Desemba, 2024, na kufafanua kuwa kozi hiyo itatolewa bure ili kutoa nafasi kwa wasichana kujitokeza kwa wingi.
Dkt. Msuya ameongeza kuwa kozi hiyo itafundishwa kwa muda wa siku 10, na baada ya kumaliza mafunzo, wahitimu watapewa vyeti vya VETA vitakavyowasaidia kuwa na sifa zinazohitajika katika soko la ajira, ambalo kwa sasa lina mvuto kwa wasichana wengi.
"Niwaombe wasichana waje kwa wingi kusoma hii kozi ili kupata ujuzi wa kutoa huduma kwenye mabasi, na zaidi tunalenga mabasi ya mikoani. Hata hivyo, tunakaribisha pia wale wanaotaka kufanya kazi kwenye daladala," anasema Dkt. Msuya.
Lengo la kozi hii ni kuwapa wasichana weredi katika kazi zao na kuwaachana na kufanya kazi hiyo kwa mazoea, jambo litakalosaidia kupandisha thamani yao kwenye soko la ajira.
Ameongeza kuwa chuo kinapokea wasichana kutoka mikoa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Songea, Mbeya, Njombe, Mwanza, Shinyanga, Kahama, Geita, Mara, Musoma, Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Manyara na Arusha.
"Nawaomba waje kwenye Chuo cha Furahika, kilichopo chini ya VETA, wapate mafunzo kuhusu njia bora za kutoa huduma ya ukondakta kwenye mabasi," anasema.
"Fani hii mwanafunzi anasoma kwa siku 10 tu, kisha tutampatia cheti cha VETA... ni bure kabisa. Hivyo tunawakaribisha watu wote wanaotaka kujifunza. Lengo ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili watu waweze kujiajiri na kuajiriwa," anasema.
Dkt. Msuya anasisitiza kuwa serikali haiwezi kutoa kila kitu kwa wananchi, na kwamba kuna mambo ambayo wananchi wanatakiwa kupigania wenyewe ili kujenga uchumi wa taifa. "Serikali haiwezi kukuletea vitu nyumbani; kuna vitu lazima sisi wenyewe tupambane kuhakikisha Tanzania ya mama Samia inawezekana kupitia kampuni zetu na ajira zinapatikana."
Anasisitiza kuwa ajira zipo, kwani wafanyabiashara na kampuni binafsi wanatoa ajira. "Hivyo, waje Furahika kusoma kozi mbalimbali tunazotoa bure kabisa," anasema.
Kozi hii ni mpya kwa wasichana wote, na inatoa fursa kwa warembo na wasichana wa darasa la saba kujifunza ujuzi muhimu wa huduma kwa wateja na vitu vinavyohitajika katika kutoa huduma kwenye magari ya usafiri.
Dkt. Msuya anasema kuwa dirisha la usajili limefunguliwa, na wanaweza kujiunga kupitia mfumo mtandao au kwa kufika chuoni hapo.
Ameongeza kuwa wanaamini kuwa kujifunza masomo mbalimbali ya VETA ni njia bora ya kumsaidia kijana kuwa na ujuzi wa maisha na kupambana na changamoto za ajira.
"Kwahiyo, tunaomba wazazi wasiwaache watoto, wawalete waje kujifunza kozi mbalimbali tunazotoa. Tunahitaji vijana wenye ujuzi ili kwenda na kasi ya soko la ajira. Kusoma tu chuo haitoshi. Kuna watu wana degree na PhD, lakini wanatembea na vyeti bila kuwa na ujuzi, na hiyo haisaidii," anasema Dkt. Msuya.
Amefafanua kuwa fursa za ajira zipo nyingi, lakini watu wengi wanashindwa kuzitumia na badala yake kuilaumu serikali.
Hakuna maoni: