TCCIA YASHIRIKIANA NA SERIKALI NA TAASISI MBALIMBALI KUKUZA MAZINGIRA YA BIASHARA NCHINI, IKAWA DARAJA LA WAFANYABIASHARA WA TANZANIA.
DAR ES SALAAM.
Serikali ya Tanzania yaendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara ili kuhakikisha sekta binafsi inachangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa taifa.
Moja wapo wa juhudi zinazofanywa na Serikali ni kupitia mashirikiano na sekta binafsi ili kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini, huku ikiwemo kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kuboresha sheria na kanuni, kuondoa vikwazo katika huduma za kibiashara, na kupunguza muda wa kupitisha mizigo.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Desemba 6, 2024 jijini Dar es salaam wakati akifungua Kongamano la Majadiliano ya Biashara na Uwekezaji kati ya Serikali na Sekta Binafsi Mwaka 2024 na Mkutano Mkuu wa 49 wa Mwaka 2024 wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).
Dkt. Biteko ameeleza umuhimu wa sekta binafsi na kusema kuwa Tanzania na Afrika kwa ujumla inakisiwa kuwa vijana wengi ambao wanaingia katika soko la ajira wanategemea sekta binafsi ndio maana Serikali imeendelea kushirikiana na kutatua changamoto za sekta binafsi.
“ Hivi karibuni mlitoa malalamiko kadhaa ikiwemo ya kukwamisha shughuli za biashara na Serikali imeyatatua kwa kushirikiana nanyi pamoja na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja baadhi ya jitihada zilizofanywa na Serikali za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini kuwa ni pamoja na kufanywa marekebisho ya sheria na kanuni 55 na sheria zingine 16 na kanuni zake zinaendelea kufanyiwa kazi.
Amesisitiza “ Serikali imeondoa mwingiliano wa majukumu na kuanzisha mamlaka mfano sasa tuna Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) ili kurahisisha shughuli zenu. Pia, imepunguza idadi ya muda wa kupata huduma kutoka siku 14 hadi tatu na kutoka siku saba hadi tatu za kusafirisha mizigo kutoka Dar es salaam hadi Tunduma.”
Pamoja na hayo Dkt. Biteko amefafanua kuwa Wakala wa Usalama Mahala Pa kazi (OSHA) imepunguza tozo 16 za biashara ambazo kupitia hizo Serikali inapoteza mapato kiasi cha shilingi bilioni 37 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi na jitihada za Rais Samia za kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Pia, amezungumzia viashiria vya ukuaji wa uchumi na kusema kuwa kumekuwepo na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme ambapo awali hayakuwahi kuzidi megawati 219 kwa mwaka na kuwa mwaka 2024 mahitaji ni megawati 420.
“ Mkifanyabiashara maana yake mahitaji ya nishati ya umeme yanaongezeka na hii ni kwa sababu viwanda vingi vimejengwa na uchumi unachangamka. Tunaanza kuona wananchi wanatumia umeme megawati 52 na viwanda vinatumia megawati 48 hii ni kiashiria kuwa uchumi unaendelea kukua vizuri,” amebainisha Dkt. Biteko.
Vilevile, amewaasa wafanyabiashara nchini kulipa kodi kwa hiari ili Serikali iweze kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali itakayosaidia utoaji huduma za kijamii kwa wananchi na kuchochea maendeleo huku akiwataka kuzalisha malighafi na bidhaa zenye ubora zitakazovutia masoko na kutoa ajira kwa watu.
“Nchi yetu tutaijenga wenyewe na tuambiane ukweli kwamba kulipa kodi ni wajibu wetu, kwa mikataba hii iliyowekwa saini hapa leo TCCIA muwe mawakala wa kutoa elimu ya mlipa kodi kwa wananchi ili watu waone heshima ya kulipa kodi,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza nchini huku akivitaka vyama vya kisekta kuepuka migogoro na kusisitiza upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwao.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo amesema kuwa Mkoa huo umekuwa na ushirikiano mzuri na TCCIA katika shughuli mbalimbali.“Wafanyabiashara hawa wamekuwa wakipongeza jitihada za Rais Samia kwa kupunguza msongamano wa meli bandarini, kuboreshwa kwa miundombinu wezeshi ya viwanda mfano zaidi ya shilingi trilioni moja imetolewa katika miradi ya barabara ya DMDP na sasa umeme uko wa kutosha na wanaendelea kufanya biashara vizuri,” amesema Mpogolo.
Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Vicent Minja kwa niaba ya wafanyabiashara nchini amempongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kuifungua nchi na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara Tanzania na hivyo kusaidia biashara kufanyika kwa utulivu.Amesema taasisi yake ina ofisi katika nchi za China, Uturuki na Uingereza na hivyo inarahisisha kuunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na nchi mbalimbali.
“Tunaishukuru Serikali kwa kurahisisha maendeleo ya biashara katika Bandari ya Dar es salaam sasa meli zikija na mizigo zinapakuwa ndani ya siku chache, pia tunamshuru Rais Samia kwa kuunda tume ya kushughulikia masuala ya kodi,” amesema Minja.
“Katika kipindi cha miaka 36 TCCIA imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha ushindani na kuvutia wadau wa ndani na nje ya nchi,” amesema Kissanga
Ameongeza kuwa lengo TCCIA ni kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo endeleo na kujenga uchumi imara huku akimpongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kuhakikisha kunakuwepo na ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi.
Kissanga ametaja baadhi ya utekelezaji wa shughuli za TCCIA katika kipindi cha mwaka 2024 kuwa kutoa mafunzo ya kuelimisha Watanzania kuhusu Soko Huru la Afrika kutoka katika mikoa nane, imesafirisha shehena za bidhaa mbalimbali katani ikiwa ni asilimia 70 ya shehena yote.
Vilevile, imefanya ukaguzi wa viwanda 37, na kufanya Jukwaa la Biashara ya Korosho Tanzania na kuleta nchini zaidi ya kampuni 100. Sambamba na kuzisaidia kampuni za Tanzania kupata fursa za uwekezaji na masoko kutoka nchi mbalimbali duniani.
Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Trademark Afrika, Elibariki Shammy amesema taasisi yake inalenga kuisaidia Watanzania na Afrika kwa ujumla ili iweze kufanyabiashara na dunia na kuwa ina wadau kutoka sekta ya umma na binafsi na hivyo wanashukuru kwa kuendelea kuaminiwa katika kutekeleza shughuli zao.
Aidha, kupitia Kongamano hilo Dkt. Biteko ameshuhudia utiaji saini wa baadhi ya mkataba ikiwemo wa shirika la Foundation for Civil Society (FCS) limeingia katika ushirikiano na TCCIA ili kukuza biashara jumuishi inayolenga watumiaji wote, wakiwemo wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Ushirikiano huo unalenga kutoa msaada wa kisheria na kiuchumi kwa makundi haya, kuhakikisha wanapata fursa za biashara, na kukuza uchumi wa kijani. FCS itasaidia TCCIA kutekeleza mikakati ya ulinzi wa watumiaji, na kutoa mafunzo kuhusu biashara endelevu na ya kijani. Mkataba huu pia utachangia katika kuongeza ufanisi wa sekta binafsi na kuhamasisha ushirikiano kati ya mashirika ya kijamii, taasisi za udhibiti, na sekta binafsi.
Rutenge Aliongeza kuwa, "Lengo letu ni kukuza mazingira ambapo sauti za jamii zinapewa kipaumbele. Ushirikiano na TCCIA ni muhimu katika kutimiza malengo haya. Ushirikiano kati ya FCS na TCCIA ni mfano muhimu wa jinsi vitendo vya pamoja vinavyoweza kuleta mabadiliko chanya.
Nae Rais wa TCCIA Vicent Minja amesisitiza kuwa, "TCCIA inajizatiti katika kusaidia biashara zote, hasa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu kuendesha biashara. Kwa kushirikiana na FCS, tunaweza kuleta mabadiliko halisi katika maisha ya wafanyabiashara hawa." Aliongeza kuwa TCCIA itashirikiana na Baraza la Biashara la Kanda na Wilaya katika kutetea ulinzi wa watumiaji na biashara jumuishi, na pia kusaidia katika kubuni mipango ya biashara na kutoa ushauri kwa biashara zinazojihusisha na biashara ya kijani.Minja alisisitiza kwamba ushirikiano na FCS utaleta mabadiliko makubwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania, "TCCIA itaratibu na Baraza la Biashara la Kanda na Wilaya kutetea ulinzi wa watumiaji na biashara jumuishi, kushiriki matokeo ya utafiti kuhusu masuala muhimu ya biashara, kuwakilisha wafanyabiashara katika majadiliano ya wizara na bunge kutetea sera ya Taifa ya Ulinzi wa Watumiaji."
Kwa hivyo, kupitia ushirikiano huu na mikataba mbalimbali, Serikali, TCCIA, na FCS wanaendeleza juhudi za kutatua changamoto za kibiashara na kuhimiza maendeleo endelevu nchini Tanzania.
Mkataba mwingine uliosainiwa ni wa kuwezesha kufanya kazi pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi, ushirikiano wa biashara kati ya TCCIA na Chuo Cha Biashara (CBE) ambapo CBE inatarajia kuwa na mitaala ya biashara ya wanagenzi na hivyo ushirikiano huo utasaidia kufikia wafanyabiashara watakaosaidia kufundisha wanafunzi.
Mkataba mwingine uliowekwa saini ni wa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wanachama wa TCCIA kulipa kodi kwa hiari kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kurahisisha ulipaji kodi na kutoa elimu ya namna kiwango na muda wa kulipa kodi.
Kongamano hilo limeongozwa na kaulimbiu “Kuongeza Ufanisi wa Majadiliano na Ushindani wa Mauzo ya Nje kwa Ustawi wa Uchumi” limehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, viongozi mbalimbali pamoja na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkataba mwingine uliowekwa saini ni wa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wanachama wa TCCIA kulipa kodi kwa hiari kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kurahisisha ulipaji kodi na kutoa elimu ya namna kiwango na muda wa kulipa kodi.
Kongamano hilo limeongozwa na kaulimbiu “Kuongeza Ufanisi wa Majadiliano na Ushindani wa Mauzo ya Nje kwa Ustawi wa Uchumi” limehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, viongozi mbalimbali pamoja na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.



Hakuna maoni: