


Dar es Salaam, Desemba 6, 2024.
Serikali ya Tanzania inatarajia kuzindua rasimu ya kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, itakayofanyika Desemba 11, 2024 katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakati wa mkutano na wahariri na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Prof. Mkumbo alieleza kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Uzinduzi huu unafanyika baada ya zoezi la ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wananchi na wadau wa maendeleo 1.17 milioni, lililofanyika kati ya Desemba mwaka jana na Oktoba mwaka huu. Wananchi walitoa maoni yao kupitia njia mbalimbali kama tafiti, ujumbe wa simu (USSD), tovuti, makongamano, na mahojiano mahsusi.
Prof. Mkumbo alifafanua kwamba uzinduzi wa Rasimu ya Dira 2050 utaendana na uzinduzi wa awamu ya pili ya kukusanya maoni ya wadau, ambayo itahusisha uhakiki wa rasimu hiyo (validation). Awamu hii itahitimishwa Januari 18, 2025, ambapo Mhe. Waziri Mkuu atapokea rasimu ya pili ya Dira 2050, iliyoboreshwa kwa maoni ya wadau.
Aliongeza kuwa kutoka Januari hadi Machi 2025, Rasimu ya Dira 2050 itajadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika vyombo mbalimbali vya serikali, ikiwa ni pamoja na Makatibu Wakuu, Tume ya Taifa ya Mipango, na Baraza la Mawaziri. Baada ya hapo, kutoka Aprili hadi Mei 2025, Rasimu hiyo itapokelewa, kujadiliwa, na kuidhinishiwa rasmi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kati ya Mei na Juni 2025.
Prof. Mkumbo aliongeza kuwa maandalizi ya Dira 2050 yanaenda sambamba na maandalizi ya Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa Maendeleo (Long-Term Perspective Plan – LTPP), ambao utaelezea utekelezaji wa maono na matamanio yaliyomo katika Dira 2050.

Akizungumza kwa niaba ya vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Bw. Deodatus Balile, alisisitiza umuhimu wa serikali kushirikiana na vyombo vya habari katika kutoa taarifa kwa wananchi na kupokea maoni kutoka kwao. Alieleza pia shauku yake ya kuona Tanzania ikiweka kipaumbele katika sekta ya viwanda na elimu bora, ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya taifa.
“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 lazima iwe chombo kinachounganisha Watanzania wote, na kuhakikisha kuwa mabadiliko ya viongozi hayasababishi mabadiliko katika vipaumbele vya taifa,” alisema Bw. Balile.
Hakuna maoni: